SIMBA HII, SVEN KAZI ANAYO,, on August 24, 2020 at 8:09 am

NA MICHAEL MAURUS UBORA wa kila mchezaji wa Simba aliyecheza mechi ya juzi dhidi ya Vital’O ya Burundi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, umekamilisha dhana nzima ya maana halisi ya kikosi kipana walichonacho Wekundu wa Msimbazi hao. Msimu uliopita, wapenzi na viongozi wa Simba walikuwa wakiwakosesha raha watani wao wa jadi, Yanga, kwa,

NA MICHAEL MAURUS

UBORA wa kila mchezaji wa Simba aliyecheza mechi ya juzi dhidi ya Vital’O ya Burundi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, umekamilisha dhana nzima ya maana halisi ya kikosi kipana walichonacho Wekundu wa Msimbazi hao.

Msimu uliopita, wapenzi na viongozi wa Simba walikuwa wakiwakosesha raha watani wao wa jadi, Yanga, kwa kuwatambia kila wakati kuwa Wekundu wa Msimbazi hao wana kikosi kipana.

Tambo zao hizo zilimaanisha kuwa Simba wana wachezaji wengi wa kiwango cha juu wanaoweza kuunda vikosi viwili vikali ambavyo vingeweza kuwapa ushindi katika kila mchezo.

Hata hivyo, hali haikuwa hivyo kwa kiwango kilichokuwa kikielezwa, kwani si wachezaji wengi waliofanikiwa kuingia katika kikosi cha kwanza.

Mechi nyingi za Simba msimu uliopita, ziliwahusisha wachezaji wale wale waliozoleka, huku wakiwa ni wachache mno waliopenyeza kikosi cha kwanza, tena wakipewa nafasi kutokana na wenye namba zao kupata majeraha au kutumikia adhabu.

Mathalani, kipa Aishi Manula, hakuwa na mpinzani kama ilivyokuwa kwa beki wa kulia, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kwa upande wa kulia.

Nafasi ya ulinzi wa kati, Wawa hakupata upinzani, huku Kannedy Juma akibadilishana na Erasto Nyoni.

Kwa upande wa kiungo mkabaji, Jonas Mkude aliendelea kutamba kabla ya baadaye kuongezewa Gerson Fraga na kuwafanya wawili hao kuunda kombinesheni ya aina yake iliyoisaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na mechi saba mkononi.

Kwa upande wa kiungo namba nane, Clatous Chama hakuwa na mpinzani, kama ilivyokuwa kwa winga wa kushoto, Luis Miquissone, huku Francis Kahata akibadilishana na Hassan Dilunga na Deo Kanda winga ya kulia.

Kwa upande wa washambuliaji wa kati, John Bocco na Meddie Kagere hawakuwa na mpinzani japo wakati mwingine mmoja wa wawili hao alikuwa akipangwa peke yake, huku mwingine akiwa nje kutegemea na mfumo wa kocha Sven Vandenbroeck.

Ni kutokana na hilo, ikiwamo kutolewa mapema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, watu wa Yanga walikuwa wakiwabeza wenzano wa Simba kuwa hawana kikosi kipana kama walivyokuwa wakitamba.

Ni kutokana na kufahamu hilo, uongozi wa Simba ulijipanga upya na kufanya usajili kwa umakini ambao leo hii umewawezesha kutimiza dhana nzima ya kikosi kipana.

Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Vital’O, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za tamasha lao la Simba Day lililohitimishwa juzi Jumamosi, hakika Wekundu wa Msimbazi hao wamethibitisha safari hii wana kikosi kipana.

Kila mchezaji ambaye aliingia uwanjani juzi, alionyesha kuwa na kiwango cha juu, hasa wale wapya waliosajiliwa hivi karibuni tayari kukinukisha msimu ujao.

Ukianza na kikosi kilichoanza kipindi cha kwanza, langoni alisimama Manula, huku kulia akisimama Kapombe, huku kushoto akiwa ni Gadiel Michael, wakati mabeki wa kati walikuwa ni Ibrahim Ame na Joash Onyango.

Viungo walikuwa ni Jonas Mkude, Larry Bwalya, Hassan Dilunga na Said Ndemla, huku washambuliaji wakiwa ni John Bocco na Bernard Morrison.

Kila mchezaji aliyeanza kipindi cha kwanza, alionyesha uwezo wa hali ya juu, huku Onyango na Ame wakicheza kwa ushirikiano na maarifa ya hali ya juu kuthibitisha kuwa safari hii Pascal Wawa na Kennedy Juma, kazi wanayo kupata nafasi ‘First Eleven’.

Kwa upande wa safu ya kiungo, Bwalya alionyesha kiwango cha juu kuonyesha kuwa safari hii kazi ipo katika eneo hilo lenye mafundi kibao.

Kwa upande wa safu ya ushambuliaji, Morrison tayari ‘ameshawaroga’ Simba, akionekana kufiti katika eneo hilo, huku akibebwa na uzoefu wake uliomwezesha kushirikiana vema na Bocco.

Pamoja na kufunga bao la kwanza la Simba, Morrison ndiye aliyemtengenezea nafasi Bocco kupachika bao la pili la timu yao.

Kwa upande wa kikosi kilichoingia kipindi cha pili, nacho kilikuwa ni moto kwani kila mchezaji alionyesha kiwango cha juu, kuanzia wale wageni na wapya.

Kikosi hicho kiliundwa na kipa Beno Kakolanya ambaye aliumia na kumpisha Ally Salum, huku beki wa kulia akiwa ni David Kameta na kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Mabeki wa kati walikuwa ni Gerson Fraga na Kennedy Juma, huku viungo wakiwa ni Muzamiru Yassin, Clatous Chama na Ibrahim Ajib, wakati washambuliaji walikuwa ni Chris Mugalu,  Charles Ilamfya na Miraji Athuman.

Japo Luis, Wawa na Kagere hawakuonekana uwanjani siku hiyo, lakini kwa kuwa uwezo waliouonyesha wale waliocheza, hakika safari hii Simba imethibitisha dhana nzima ya kuwa na kikosi kipana, kwani kila atakayepangwa, ana uwezo wa kufanya mambo.

Akizungumzia kikosi chake kwa ujumla, Sven alisema kuwa bado ana kazi ya kuwanoa zaidi vijana wake ili kuwa moto zaidi.

“Walicheza vizuri, lakini kwa upande wangu, nimebaini kasoro kadhaa ambazo nitazifanyia kazi kwa muda huu uliobaki kabla ya kuanza kwa ligi,” alisema.

Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Agosti 30, mwaka huu, wanakabiliwa na mchezo wa ufunguzi wa msimu wa Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo FC, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Mbali ya mchezo huo pamoja na kipute cha Ligi Kuu Bara, Simba wataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *