SIMBA YAPIGA 8,, on August 27, 2020 at 7:46 am

NA ASHA KIGUNDULA KIKOSI cha Simba kimeendelea kudhihirisha ubora wake baada ya jana kutikisa nyavu za wapinzani wao mara nane ndani ya mechi mbili za kirafiki zilizopigwa kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, Dar es Salaam. Wikiendi iliyopita, Wekundu wa Msimbazi hao walitoa kipigo cha mabao 6-0 kwa Vital’O ya Burundi katika mchezo wa kuhitimisha,

NA ASHA KIGUNDULA

KIKOSI cha Simba kimeendelea kudhihirisha ubora wake baada ya jana kutikisa nyavu za wapinzani wao mara nane ndani ya mechi mbili za kirafiki zilizopigwa kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, Dar es Salaam.

Wikiendi iliyopita, Wekundu wa Msimbazi hao walitoa kipigo cha mabao 6-0 kwa Vital’O ya Burundi katika mchezo wa kuhitimisha tamasha lao la Simba Day, kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini.

Ikiwa ni moja ya maandalizi ya mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo itakayopigwa Jumapili hii Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Simba jana asubuhi ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Transit Camp na KMC.

Katika mchezo wa kwanza dhidi ya KMC, Simba ilioshinda mabao 3-1, wafungaji wao wakiwa ni Clatous Chama dakika ya 28, Ibrahim Ajib (dk.33) na Muzamiru Yassin (dk.57).

Mchezo uliofuatia dhidi ya Transit Camp, Wekundu wa Msimbazi hao walishinda 5-2, wafungaji wakiwa ni Cyprian Kipenya aliyepiga mawili, dakika ya 4 na 42, Charles Llamfya (dk.19), Meddie Kagere (dk.42) na Gadiel Michael dakika ya 79, hivyo kufanya jumla ya mabao waliyofunga Simba jana kuwa nane.

Ukiachana na hilo la ushindi na mabao kwa ujumla, upacha wa Chama na Ajib, umeendelea kila mmoja akicheka na nyavu, ukiwa ni mwendelezo wa makali yao wanaokuja nao msimu huu.

Katika toleo la BINGWA la Jumatatu, tuliripoti juu ya mkakati wa Chama kumfanya Ajib kuwa na namba kikosi cha kwanza cha Simba, akiamini Mtanzania huyo ana kipaji cha hali ya juu.

Simba ilipovaana na Vital’O Jumamosi iliyopita, Chama alifunga na Ajib naye alitikisa nyavu, huku jambo la kipekee kila mmoja akiwa ndiye aliyemtengenezea mwenzake pasi ya bao (assist).

Imeelezwa kuwa Chama amekuwa akimwapa moyo Ajib wa kupambana akimsisitia kuwa ana kipaji cha hali ya juu kuliko mchezaji mwingine yeyote wa Tanzania kwa sasa.

Mbali ya wawili hao, katika mechi zote mbili za jana, wachezaji wa Simba kila aliyepata nafasi ya kucheza, alionyesha kiwango cha hali ya juu, kuanzia wale wa kigeni hadi wazawa.

Kwa upande wa wapya wanaotupiwa zaidi macho, kiungo kutoka Zambia, Larry Bwalya, alionyesha kiwango cha juu katika kupiga pasi zenye macho, huku pia akiwa ni fundi wa kupora mipira.

Naye Bernard Morrison, hakuwa nyuma, akionyesha cheche zake kama ilivyo kawaida yake na kutoa bonge la burudani kwa benchi la ufundi na mashabiki wachache waliokuwa wakishuhudia mechi hizo.

Kati ya wachezaji wote wapya wa Simba, Joash Onyango ambaye awali alionekana kutowateka mashabiki wa klabu hiyo, beki huyo wa kati kutoka Kenya, amezidi kuwapagawisha Wanamsimbazi kutokana na utulivu na umakini wake awapo dimbani.

Kama ilivyokuwa dhidi ya Vital’O Jumamosi iliyopita, ndivyo alivyofanya jana kwani Mkenya huyo alicheza vizuri mno na kuthibitisha kuwa Wekundu wa Msimbazi hawakukosea kumsajili.

Kwa ujumla, maandalizi ya Simba kuelekea mchezo wao wa Jumapili wa Ngao ya Jamii na Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika, yanaendelea vizuri chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck na msaidizi wake, Seleman Matola.

Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi hao, zinasema kuwa kikosi cha Sven kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam Jumamosi kuelekea Arusha tayari kuivaa Namungo FC Jumapili.

Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, Simba itafungua pazia dhidi ya Ihefu, mchezo utakaochezwa Septemba 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Wakati huo huo, mchezaji wa mpya wa Simba, Chris Mugalu, juzi aliondoka nchini kwenda kwao DR Congo , akitarajia kurejea mapema wiki ijayo.

Chanzo kutoka ndani ya Simba, kimesema kuwa mchezaji huyo amekwenda kwao kwa ajili ya mambo ya kifamilia.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *