SISI NDIYO WANANCHI,, on August 27, 2020 at 7:40 am

NA ZAINAB IDDY SISI ndiyo wananchi. Hiyo ni kauli ya Wanayanga iliyokuja baada ya mapokezi ya aina yake aliyoyapata kiungo wao mpya, Carlos Carlinhos, raia wa Angola. Carlinhos alitua nchini juzi na kupokewa na umati wa mashabiki na wanachama wa Yanga waliojitokeza kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.,

NA ZAINAB IDDY

SISI ndiyo wananchi. Hiyo ni kauli ya Wanayanga iliyokuja baada ya mapokezi ya aina yake aliyoyapata kiungo wao mpya, Carlos Carlinhos, raia wa Angola.

Carlinhos alitua nchini juzi na kupokewa na umati wa mashabiki na wanachama wa Yanga waliojitokeza kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Baada ya kumpokea kwa mbwembwe, umati huo ulimsindikiza kwa kila aina ya shangwe huku wakiliimba jina lake na wadhamini wao, Kampuni ya GSM kutoka uwanjani hapo hadi makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani, jijini.

Shangwe zaidi zilikuwa ni pale msafara huo ulipofika Mtaa wa Msimbazi, yalipo maskani ya watani wao wa jadi, Simba ambako idadi ya mashabiki wa klabu hiyo iliongezeka na kuzua bonge la msongamano wa magari.

Walipofika makao makuu yao, idadi ya mashabiki ilikuwa ni kubwa zaidi na kuripuka shangwe ya aina yake kuonyesha jinsi Wanajangwani hao walivyokuwa wakimsubiri kwa hamu kiungo huyo.

Na sasa wakati baadhi wakiwashangaa watu wa Yanga kwa mapokezi ya aina ile kwa mchezaji mmoja tu, wenye klabu yao wametamba kuwa hiyo ndiyo tafsiri ya dhana nzima ya neno Wananchi.

Akizungumza na BINGWA jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Yanga, Hassan Bumbuli ‘HB’, alisema kuwa mapokezi yale ni salamu kwa wapinzani wao, akiwamo nyota wao ‘aliyekimbilia’ Simba, Bernard Morrison.

“Hii ndiyo maana ya Wananchi, Yanga ina mashabiki wenye mapenzi ya kweli na klabu yao, wakipenda… wamependa kweli, siku zote hutanguliza uzalendo kwanza, mengine huja baadaye.

“Unaweza kuliona hilo hata katika mechi zetu, timu inaweza isifanye vizuri, lakini bado mashabiki watatumia fedha zao na kusafiri kuifuata popote inapokwenda kucheza.

“Juu ya mapokezi ya Carlonhos, tunataka kuwaonyesha wapinzani wetu kuwa Wananchi wanapoamua jambo lao, lazima lifanikiwe. Tuliposema tunamleta kiungo kutoka Angola, kuna watu walikuwa wakikataa. Hivyo alipotua, tumewaziba midomo,” alisema.

Aliongeza: “Lakini mapokezi yale pia ni salamu kwa wachezaji wanaotusumbua na wasioiheshimu nembo ya Yanga. Hebu muulizeni huyo anayetusumbua (Morrison), yeye na Carlonhos, nani amepewa heshima zaidi?”

Ikumbukwe kuwa BINGWA ndilo lililokuwa gazeti la kwanza kuripoti juu ya ujio wa Carlinhos Yanga, baada ya kupenyezewa habari hiyo na mmoja wa watu wa karibu na kigogo wa GSM, anayeshughulikia usajili, Mhandisi Hersi Said.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umesema kuwa Jumapili katika kilele cha tamasha lao la Wiki ya Wananchi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, kutakuwa na bonge la ‘surprise’.

Japo uongopzi wa Yanga umeshindwa kuweka wazi juu ya ‘surprise’ hiyo, lakini BINGWA limetonywa kuwa kuna uwezekano klabu hiyo ikamshusha mshambuliaji hatari raia wa Rwanda, Jacques Tuyisenge.

Tuyisenge aliyewahi kuichezea Gor Mahia ya Kenya, kwa sasa anakipiga katika klabu ya Petro de Luanda iliyopo Ligi Kuu Angola.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga jana kiliendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Dar es Salaam, ikiwamo kucheza mchezo wa kirafiki na African Sports ya Tanga.

Katika mchezo huo, Yanga ilishinda mabao 2-1, wafungaji wa Wanajangwani hao wakiwa ni Deus Kaseke na Adeyum Saleh, wakati lile la Wana Kimanumanu, likiwekwa kambani na James Mendi.

Katika mchezo huo, nyota wapya wa kigeni wa Yanga, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda na Michael Sarpong, walicheza vizuri na kuwapagawisha viongozi wao waliokuwapo uwanjani hapo.

Mukoko na Tuisila waliwakosha viongozi wao, akiwamo Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Mhandisi Hersi Said, Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla na makamu wake, Fredrick Mwakalebela ambao mara kwa mara walionekana kuinuka vitini huku wakiwapigia makofi.

Kipindi cha pili, kocha wa viungo, Riedoh Berdien ambaye ndiye mwongozaji wa mazoezi ya timu hiyo tangu yalipoanza wiki iliyopita, alifanya mabadiliko kwa kumtoa Kisinda na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Mussa, kabla ya kuwaingiza Sarpong, Haruna Niyonzima na Bakari Mwamnyeto na kuibua shangwe kwa watazamaji.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *