Posted By Posted On

Simba wanabeba mataji tu,, on August 31, 2020 at 9:11 am

NA ZAINAB IDDY, ARUSHA SIMBA wameanza msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kutwaa Ngao ya Jamii,  baada ya kuifunga mabao 2-0 Namungo katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid,  jijini hapa. Katika mchezo huo, uliochezeshwa na mwamuzi Ramadhan Kayoko,  Simba  walipata bao la kuongoza lililofungwa na John Bocco kwa mkwaju,

NA ZAINAB IDDY, ARUSHA

SIMBA wameanza msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kutwaa Ngao ya Jamii,  baada ya kuifunga mabao 2-0 Namungo katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid,  jijini hapa.

Katika mchezo huo, uliochezeshwa na mwamuzi Ramadhan Kayoko,  Simba  walipata bao la kuongoza lililofungwa na John Bocco kwa mkwaju wa penelti,  baada ya Mghana Bernard Morrison kuchezewa rafu ndani ya eneo la hatari na beki wa Namungo, Hamis Fakhi.

Bocco alipachika bao hilo dakika ya saba, kabla ya Morrison  kufunga la pili dakika ya 60, baada ya kupokea pasi ya mwisho kutoka kwa Clatous Chama.

Msimu uliopita, Simba walianza kwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga mabao 4-2 Azam kwenye Uwanja wa Mkapa na baadaye kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba walifunga msimu kwa kutwaa taji la tatu la michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), baada ya kuifunga mabao 2-1 Namungo katika mchezo wa fainali uliochezwa Agosti 2, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Mchezo wa jana ulianza kwa kasi huku kila timu ikitaka kupata bao la kuongoza, lakini ilikuwa Simba iliyotangulia kupata bao na baadaye kuongeza la pili  na kudumu hadi dakika 90.

Katika mchezo huo, Namungo walikuwa wa kwanza kufika langoni kwa Simba dakika ya tatu, lakini mkwaju wa Sixtus Sabilo ulipanguliwa na kipa wa Simba, Aishi Manula.

Kiungo wa Simba Chama alikosa bao dakika ya nne baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa wa Namungo, Nourdin Barola, kabla ya mpira kumkuta Morrison, aliyeachia shuti kali na kutoka  nje.

Namungo ilipoteza nafasi ya kufunga dakika ya 17, lakini mchezaji wake, Steven Sey alipiga shuti hafifu na Manula kudaka.

Simba iliendelea kutawala mchezo na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni kwa timu ya Namungo ambayo, ilikubali kichapo hicho.

Hata hivyo, Steven Sey alishindwa kuifungia timu yake ya Namungo dakika ya 37, baada ya kupokea  pasi ya Sabilo, lakini shuti lake liliyopanguliwa na Manula na mpira kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Mwamuzi Kayoko alimwonyesha kadi ya njano Morrison, ikiwa ni dakika ya 40,  baada ya kumfanyia madhambi beki wa Namungo Fakhi.

Naye  Kocha wa timu ya  Simba, Mbelgiji  Sven Vandenbroeck alionyeshwa kadi ya njano  dakika ya 45, baada ya kupinga uamuzi wa Kayoko.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili, Simba waliingia uwanjani kwa lengo la kuongeza bao lingine na kufanikiwa malengo yao katika mchezo huo.

Simba; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’,  Joah Onyango, Kennedy Juma, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/David Kameta (dk.78), Mzamir Yassin, John Bocco/Meddie Kagere (dk.78), Clatous Chama/ na Bernard Morrison/Larry Bwalya (dk.67).

Namungo; Nourdine Balora,  Rodgers Gabriel/Haruna Shamte (dk.63),  Jaffar Mohamed, Steven Duah, Hamisi Fakhi/Hamis Khalfan (dk.3), Abdulhalm Humud/Aman Kyata, Abeid Athumani/Bigirimana Blaise (dk.46), Lucas Kikoti, Steven Sey, Nzigamasabo Steve na Sixtus Sabilo/Shiza Kichuya (dk.46).

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *