Posted By Posted On

WAPE SALAAM,, on August 31, 2020 at 9:08 am

NA ASHA KIGUNDULA HII ndiyo Yanga ya kimataifa. Walichokitaka mashabiki ndicho walichokipata. Hakuna aliyesononeka. Naam! Maelfu ya mashabiki waliojitokeza Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu wa Nne, Jakaya Kikwete, walipata burudani wa kutosha katika kilele cha Wiki ya Wananchi iliyohitimishwa jana kwa mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya,

NA ASHA KIGUNDULA

HII ndiyo Yanga ya kimataifa. Walichokitaka mashabiki ndicho walichokipata. Hakuna aliyesononeka.

Naam! Maelfu ya mashabiki waliojitokeza Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu wa Nne, Jakaya Kikwete, walipata burudani wa kutosha katika kilele cha Wiki ya Wananchi iliyohitimishwa jana kwa mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya wenyeji Yanga na Aigle Noir ya Burundi.

Milango ya Uwanja wa Mkapa ilifunguliwa kuanzia mida ya saa tatu asubuhi lakini ilipotimia saa moja usiku ndipo sherehe hizo zikahitimishwa na mchezo mkali wa kimataifa.

Walikuwa wenyeji Yanga ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 lakini kilichoonekana kuwafurahisha zaidi mashabiki wa timu hiyo ni soka la kiwango cha juu walichokionyesha wachezaji wa Yanga.

Mabao yote ya Yanga yaliwekwa kimiani na wachezaji wao wapya na wote raia wa kigeni; Tuisila Kisinda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Mghana Michael Sarpong.

Yalikuwa ni mabao mazuri ambayo yaliwafanya mashabiki wa Yanga kusikika wakisema hiyo ndiyo ‘salamu za kidigitali’.

Yanga walionyesha mchezo ambao uliendana na ujumbe wa Rais Mstaafu Kikwete ukiwataka warudishe ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu walioupoteza kwa mahasimu wao Simba.

Ilimchukua dakika 38 tu kwa Tuisila kufungua akaunti yake ya mabao Yanga baada ya kuonyesha utulivu alipopokea pasi safi ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kumuona kipa amekaa vipi golini kabla ya kupiga shuti lililojaa wavuni.

Sarpong ambaye anaonekana wazi ndiye atakayekuwa chaguo la kwanza kuongoza mashambulizi Yanga, alikuwa sehemu sahihi katika wakati sahihi na kufunga kwa kichwa bao nzuri la pili la Yanga dakika ya 51.

Ni ushindi ambao Wanayanga wanajitamba timu yao sasa imeiva kwa Ligi Kuu Bara huku wakisema yeyote atakayekatiza mbele yao atakiona cha moto.

Mbali na ushindi huo, Yanga waliutawala mchezo huo na miongoni mwa wachezaji waliyowafurahisha mashabiki kutokana na uwezo wa umiliki mpira na chenga ni Tuisila na Fei Toto.

Wageni Aigle Noir walijikuta wakilazimika kucheza pungufu kwa zaidi ya dakika 60 baada ya mchezaji wao, Koffi Kwassi, kuonyesha kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya kutokana na utovu wa nidhamu.

Awali, Saanya alikuwa ameshamuonya mchezaji huyo kwa kadi ya njano baada ya kuchezea vibaya Deus Kaseke lakini dakika ya 30 alionyeshwa kadi ya pili ya njano.

Baada ya hitimisho wa Wiki ya Wananchi na ushindi mzuri wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir, Yanga sasa wanaelekeza mawazo yao kwa mechi yao ya ufunguzi Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons mwishoni mwa wiki hii.

Kikosi cha Yanga: Metacha Mnata/Faruk Shikhalo(dk 60),  Mbwana Shomari, Yassin Mustapha,  Abdallah Shaibu/Carlinhos (dk 81), Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarphong, Ditram Nchimbi na Deus Kaseke.

Aigle Noir: Eric Maola,  Naikumana Merci, Honemuou Desire, Hitimana Hamza, Masudi Marcisse, Koffi Kwassi,  Ndikumana Asman, Nga Bobibza, Charist Attegbe na Nzojibwani Frank.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *