Posted By Posted On

YACOUBA MABAO ATUA DAR,, on September 1, 2020 at 6:45 am

NA WINFRIDA MTOI MSHAMBULIAJI hatari wa Asante Kotoka ya Ghana mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao, Yacouba Songne, ametua jijini Dar es Salaam tayari kuanza kuhamishia cheche zake za kucheka na nyavu Yanga. Yacouba aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu na Wanayanga, alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana mchana,

NA WINFRIDA MTOI

MSHAMBULIAJI hatari wa Asante Kotoka ya Ghana mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao, Yacouba Songne, ametua jijini Dar es Salaam tayari kuanza kuhamishia cheche zake za kucheka na nyavu Yanga.

Yacouba aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu na Wanayanga, alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana mchana na kupokewa na viongozi na wapenzi wa Yanga.

Kama ilivyo kawaida yao, wapenzi wa Yanga walijitokeza kwa wingi uwanjani hapo kumpokea straika wao huyo, huku wakionekana kuwa na furaha kutokana na kiwango walichoonyesha nyota wao wapya juzi katika kilele cha tamasha lao la Wiki ya Wananchi.

Katika tamasha hilo lililohitimishwa kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini, wachezaji wapya wa Yanga walionyesha kiwango cha juu na kuwafanya wapenzi wa klabu hiyo kuwa na furaha isiyo na kifani.

Na jana Yacouba aliendeleza furaha yao baada ya straika huyo raia wa Burkina Faso kutua nchini, tayari kuunda safu hatari ya ushambuliaji ya Yanga sambamba na Mghana Michael Sarpong na winga matata raia wa DR Congo, Tuisila Kisinda.

Yacouba alitakiwa kutua tangu Ijumaa ya wiki iliyopita na kuwafanya wapenzi wa Yanga kusota Uwanja wa Ndege bila mafanikio.

Akizungumza Uwanja wa Ndege baada ya kumpokea Yacouba, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mhandisi Hersi  Said, alisema sababu ya kuchelewa kwa mchezaji huyo ni utaratibu mgumu wa usafiri kutokana na hali iliyopo kwa sasa.

“Leo (jana) tumekuja kumpokea mchezaji wetu, Yacouba Songne, usajili tulikuwa tukiusubiri na namtambulisha rasmi kuwa mchezaji wa Yanga, tulitakiwa kuwa naye katika Wiki ya Wananchi, lakini usafiri kule kwa ulikuwa mgumu,” alisema.

Kwa upande wake, mchezaji huyo hakuzungumza maneno mengi bali aliahidi kuifungia mabao timu hiyo na kuwashikuru mashabiki walijitokeza kumlaki.

“Nimekuja Tanzania ili kuisaidia timu yangu mpya ya Yanga, jukumu langu lililonileta hapa ni kufunga mabao, sitawaangusha mashabiki nashukuru sana kwa mapokezi haya makubwa,” alisema Yacouba.

Baada ya kutoka uwanjani hapo, Yacouba alipelekwa makao makuu ya Yanga yaliyopo Jangwani, jijini na kukabidhiwa jezi namba 10.

Yacouba anakuwa mchezaji wa tano mpya wa kigena wa Yanga, akiungana na akina Sarpong (Ghana), Carlos Carlinhos (Angola), Tuisila na Tonombe Mukoko wote kutoka DR Congo.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *