Posted By Posted On

NI YEYE,, on September 4, 2020 at 10:31 am

NA ZAINAB IDDY WAKATI Tuisila Kisinda, Mukoko Tunombe, Carlos Carlinhos na Yacouba Songne, wakiwa ndio wachezaji wapya wa Yanga waliotikisa zaidi, kwa upande wa Simba, unaambiwa wakali hao wala hawajawashtua kivile, wakiwaona wa kawaida tu. Itakumbukwa kuwa kati ya wachezaji wapya wa Yanga wa kigeni, Carlinhos ndiye aliyetikisa zaidi, akipata mapokezi ya kufa mtu alipotua,

NA ZAINAB IDDY

WAKATI Tuisila Kisinda, Mukoko Tunombe, Carlos Carlinhos na Yacouba Songne, wakiwa ndio wachezaji wapya wa Yanga waliotikisa zaidi, kwa upande wa Simba, unaambiwa wakali hao wala hawajawashtua kivile, wakiwaona wa kawaida tu.

Itakumbukwa kuwa kati ya wachezaji wapya wa Yanga wa kigeni, Carlinhos ndiye aliyetikisa zaidi, akipata mapokezi ya kufa mtu alipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Carlinhos aliyejiunga na Yanga akitokea klabu ya G.D. Interclube ya Angola, alianza kuteka hisia za Wanayanga baada ya gazeti hili, katika toleo la Agosti 18, mwaka huu kuripoti kwa mara ya kwanza juu ya ujio wake kwa wakali hao wa Jangwani.

Tangu hapo Wanayanga na wapenzi wa soka nchini wakaanza kumfuatilia kiungo huyo na kufahamu ni bonge la kiungo, hivyo siku alipotua nchini, alipata mapokezi ya aina yake.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Tuisila, Mukoko na hata Yacouba walipotua nchini kuanza kuitumikia Yanga.

Lakini kati yao, kuna mkali ambaye hakuwa amepata mapokezi makubwa kama wenzake hao ambaye ndiye hasa anayewakosesha usingizi Simba, huyo si mwingine bali ni Michael Srapong.

Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa Srapong wanamwona kama mchezaji hatari zaidi wa Yanga kuelekea msimu huu wa 2020/21 ambaye watahitaji kuwa makini naye.

Ikumbukwe kwa Simba nao walikuwa wakimtaka mshambuliaji huyo aliyekuwa akikipiga Rayon Sports ya Rwanda, lakini baadaye walighairi na kuhamia kwa Chriss Mugalu wa Lusaka Dynamos ya Zambia.

Lakini kutokana na kiwango alichokionyesha Sarpong, Yanga ilipovaana na Aigle Noir ya Burundi Jumapili iliyopita katika mchezo wa kirafiki wa tamasha lao la Wiki ya Wananchi, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, watu wa Simba wamebaini mchezaji huyo ni moto wa kuotea mbali.

Mmoja wa viongozi wa Simba aliyepo katika Kamati ya Utendaji aliyekataa jina lake kuwekwa wazi, ameliambia BINGWA kuwa kati ya mambo yaliyowatisha kwa Sarpong, ni uwezo wake wa kupambana na mabeki, lakini pia matumizi yake mazuri ya kichwa kufunga mabao.

“Japo tulikuwa tukicheza Arusha (Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo), macho yetu tuliyaelekeza Uwanja wa Mkapa kuona viwango vya wachezaji wapya wa Yanga. Kati ya wote waliosajiliwa msimu huu, Sarpong anaonekana kuwa tishio zaidi.

“Ana nguvu za kupambana na mabeki, ana kasi na anajua jinsi ya kujipanga. Lakini pia bao alilofunga, limeonyesha kuwa ni tishio, kwa wachezaji wetu tuliowazoea, hawezi kufunga bao kwa kichwa kama vile, tena akipiga akiwa mbali ya goli. Mpira wa kichwa lakini unaweza kusema kapiga kwa mguu!

“Tumeshamjulisha kocha (Sven Vandenbroeck) amwangalie vizuri Sarpong kupitia mchezo ule wa Jumapili na mechi zake alizowakuwa akicheza huko alikotoka, kisha aone nini cha kufanya na mabeki wake,” alisema.

Mtoa habari wetu huyo ameungwa mkono na kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah ‘King’ Kibaden, aliyesema kuwa Sarpong raia wa Ghana, ni moja ya usajili bora uliofanywa na Yanga hivi karibuni.

Akizungumza na BINGWA jana, Kibaden anayeshikilia rekodi ya kupiga ‘hat-trick’ katika pambano la watani, Simba ilipoichapa Yanga mabao 6-0 mwaka 1977, alisema ukubwa wa umbo la Sarpong, unambeba katika kutimiza majukumu yake, hasa anapokutana na mabeki wenye maumbo madogo.

“Nimevutiwa sana na usajili wa Yanga kwa Sarpong, kwangu ni mchezaji mwenye sifa zote za kocha kujivunia, tukianzia katika umbo alilonalo.

“Niliona katika mechi ya Wiki ya Wananchi, ameonyesha nini ambacho anacho katika miguu yake, ana kasi, nguvu na jicho kali la kuona bao, ni mchezaji mahiri sana, Yanga wakimuamini na kumpa nafasi, atakuwa msaada kwao kwa kufunga mabao mengi,” alisema.

Kibaden alisema ili Sarpong awe mzuri zaidi, anatakiwa kuboresha ‘movement’ zake kwenye eneo la mwisho ili kuipa matunda mazuri Yanga.

Akizungumzia matarajio yake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaoanza keshokutwa, Kibaden alisema utakuwa mgumu kwa sababu kila timu imejipanga kuleta mageuzi katika soka la Tanzania.

“Ligi itakuwa ngumu hasa, bila shaka hadi mzunguko wa kwanza unamalizika, itakuwa tayari imeshajulika nani analitaka taji na timu zipi zitashuka daraja kulingana na kile ambacho watakifanya katika michezo yao ya mwanzo,” alisema.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *