Posted By Posted On

SIMBA WALA KIAPO,, on September 4, 2020 at 10:03 am

NA WINFRIDA MTOI KAMA kuna klabu ambayo inadhani inaweza kutwaa kirahisi ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa 2020/21, basi itatakiwa kujipanga hasa kwani mabingwa watetezi, Simba wameapa kutokubali kulipoteza taji lao hilo. Mbali ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara wanaoushikilia kwa msimu wa tatu mfululizo, Simba imepanga kutoa vipigo kwa kila timu,

NA WINFRIDA MTOI

KAMA kuna klabu ambayo inadhani inaweza kutwaa kirahisi ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa 2020/21, basi itatakiwa kujipanga hasa kwani mabingwa watetezi, Simba wameapa kutokubali kulipoteza taji lao hilo.

Mbali ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara wanaoushikilia kwa msimu wa tatu mfululizo, Simba imepanga kutoa vipigo kwa kila timu watakayokutana nayo katika michuano yote watakayoshiriki, ikiwamo Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na ile ya kimataifa.

Kati ya mambo ambayo yamekuwa yakiwapa Simba jeuri ya tambo zao hizo, ni usajili waliofanya msimu huu, wakiwanasa wachezaji wanaoamini ni wa kiwango cha juu kutoka sehemu mbalimbali.

Kwa hapa nchini, Simba imesajili wazawa wapya wawili ambao ni Charles Ilanfya kutoka KMC, David Kameta (Lipuli) na Ibrahim Ame (Coastal Union), huku wa kigeni wakiwa ni Bernard Morrison (Yanga, Ghana), Larry Bwalya (Power Dynamos, Zambia), Chriss Mugalu (Lusaka Dynamos, Zambia) na Joash Onyango (Gor Mahia, Kenya).

Ukiachana na hilo la wachezaji, ubora wa benchi la ufundi chini ya kocha Sven Vandenbroeck na msaidizi wake, Seleman Matola pamoja na uongozi imara wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo’ nao umechangia mkwara huo wa Simba.

Tayari Wekundu wa Msimbazi hao wameufungua msimu mpya kwa mbwembwe baada ya kutwaa Ngao ya Jamii wikiendi iliyopita, kwa kuichapa Namungo FC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Kuelekea mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Bara 2020/21 dhidi ya Ihefu keshokutwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, Simba tayari wameshatua jijini humo tangu Jumanne kuhakikisha wanaianza ligi kwa kishindo.

Katika kusisitiza mkakati wao huo wa kutoacha kitu 2020/21, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, pamoja na kuamini msimu huu hautakuwa rahisi, lakini hilo halitawazuia kuzoa pointi tatu Jumapili.

Akizungumza baada ya mazoezi ya jana kwenye Uwanja wa Sokoine, Sven alisema: “Ni msimu mwingine wa Ligi Kuu tunauanza, tumejipanga vizuri, tunaingia tukiwa na njaa ya pointi, lengo letu ni moja la ushindi kupigania timu kuendeleza kile tulichokianza.”

Alisema katika kikosi chake, kila mchezaji ni bora, kitu kinachomfanya awe na machaguo mengi ya kupanga  timu kulingana na mfumo anaotaka kuutumia.

Kocha huyo alisema haifahamu Ihefu na hana taarifa zao, lakini kilichopo kichwani mwake na kwa wachezaji wake ni kupambana kusaka ushindi.

Naye Meneja wa kikosi hicho, Patrick Rweyemamu,  alisema kuwa katika timu yao, hakuna tatizo lolote kati ya benchi la ufundi na wachezaji, kila mmoja akili yake akiielekeza katika mechi zinazowakabili.

“Sisi akili yetu yote ipo kwenye ligi, hatuwezi kuvurugwa na maneno ya watu, tunajua tunachokifanya, kikubwa ni kuhakikisha tunaendelea kuwa kama msimu uliopita,” alisema Rweyemamu.

Alisema Ihefu wengi wanaichukulia kama ni kibonde,   lakini wao wataingia uwanjani wakijua wanakwenda kukutana na timu bora inayoshiriki Ligi Kuu Bara kama ilivyo Simba.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *