Posted By Posted On

BAADA YA MECHI TANO… YANGA HII MTAIKOMA,, on September 7, 2020 at 6:57 am

NA ASHA KIGUNDULA YANGA imeianza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21 kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam jana, huku wachezaji wake wapya waliocheza, Michael Sarpong, Mukoko Tonombe na wengineo wakionyesha kiwango cha juu. Mbali ya wawili hao, wengine wapya walioonyesha,

NA ASHA KIGUNDULA

YANGA imeianza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21 kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam jana, huku wachezaji wake wapya waliocheza, Michael Sarpong, Mukoko Tonombe na wengineo wakionyesha kiwango cha juu.

Mbali ya wawili hao, wengine wapya walioonyesha cheche zao jana ni mabeki wa pembeni, Yassin Mustafa na Kibwana Shomari, huku Bakari Mwamnyeto naye akitulia vema beki ya kati.

Pia, Tuisila Kisinda alionyesha kiwango cha juu baada ya kuingia kipindi cha pili, kama ilivyokuwa kwa Farid Musa ambaye alicheza vizuri mno.

Kwa ujumla, tofauti na ilivyotarajiwa na wengine, kikosi cha Yanga kilicheza vizuri, kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kukubali kuwa idadi kubwa ya wachezaji walikuwa ni wapya ambao hawajakaa pamoja kwa muda mrefu.

Idadi kubwa ya wachezaji wapya wa Yanga, hasa wa kigeni, Mukoko, Sarpong na Tuisila, walitua Yanga takribani wiki mbili kabla ya ligi kuanza, huku Yacouba Songne ambaye naye jana alicheza, akiwasili wiki iliyopita.

Ukiachana na hilo, hata kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic, hajapata muda wa kutoa nondo zake kwa wachezaji wake kwani naye alitua Jangwani wiki moja kabla ya ligi kuanza.

Kwa ujumla, pamoja na kuambulia sare, kikosi cha Yanga kilicheza vizuri na kuibana vilivyo Prisons iliyokuwa pamoja kwa muda mrefu, hasa dakika za mwisho, kiasi cha wapinzani wao hao kutamani mchezo umalizike.

Hadi mchezo huo unamalizika, wapenzi wa Yanga waliokuwapio uwnajani hapo, walitoka wakiwa na nyuso za furaha, wakiamini baada ya vijana wao kuzoeana na kupewa maufundi na Zlatko, watakuwa ni moto wa kuotea mbali.

Walikuwa ni Tanzania Prisons walioanza kuliona lango la Yanga dakika ya 7, mfungaji wao akiwa ni Lambart Sabianka aliyeachia shuti kali lililotinga nyavuni baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mohammedi Mkopi.

Yanga walisawazisha bao hilo dakika ya 18 kupitia kwa Sarpong, aliyeachia shuti kali akiwa ndani ya sita baada ya shambulizi la nguvu lililoanzia winga ya kushoto kutoka kwa Farid.

Ukiachana na mabao hayo, timu zote mbili zilipoteza nafasi kadhaa, japo kwa upande wa Yanga, zilikuwa nyingi zaidi.

Dakika ya 13, Sarpong alikaribia kuipa Yanga bao, lakini alishindwa kumalizia pasi maridadi kutoka kwa Shomari

Dakika tano baadaye, Sarpong aliwainua wapenzi wa Yanga kwa kufunga bao lake la kwanza Ligi Kuu Bara tangu atue Jangwani.

Mchezaji Adilly Buha wa Tanzania Prisons, alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 39 baada ya kumchezea vibaya Sarpong.

Hadi dakika 45 za mchezo huo zinamalizika, timu hizo zilitoka uwanjani zikiwa zimefungana bao 1-1.

Yanga walikianza kipindi cha pili kwa kasi, ikiwa ni baada ya kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Farid nafasi yake kuchukuliwa na Tuisila, huku Deus Kaseke akimpisha Yacouba.

Prisons nao walifanya mabadiliko dakika ya 52, wakimtoa Adilly Buha na nafasi yake kuchukuliwa na Ezekia Mwashilindi.

Dakika ya 55, Ditram Nchimbi alikosesha Yanga bao baada ya kushindwa kumalizia krosi ya Bakari Mwamnyeto, tena akiwa katika nafasi nzuri ndani ya 18. 

Dakika ya 62, Mwashilindi nusura aifungie Prisons bao, lakini akiwa yeye na kipa wa Yanga, Farouk Shikalo, alipiga shuti lililotoka nje.

Baada ya kosakosa hiyo ya Prisons, Yanga walicharuka na kulishambulia lango la wapinzani wao hao.

Shambulizi hilo nusura liipatie Yanga bao dakika ya 65, lakini akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, Tuisila alishindwa kucheka na nyavu kwa shuti lake kwenda nje.

Dakika ya 76, timu zote zilifanya mabadiliko, Yanga ikiwatoa Mauya na nafasi yake kuchukuliwa na Mukoko, huku na Prisons ikimwingiza Kassim Mdoe kuchukua nafasi ya Salum Kimenya.

Dakika ya 81, mwamuzi Emannuel Mwandembwa kutoka Arusha, alimtoa Nurdin Chona kwa kadi nyekundu, baada ya kumchezea vibaya Yacouba na kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

Yanga walikosa nafasi tatu za mabao dakika tano za mwisho kutokana na washambuliaji wake kutokuwa watulivu, hilo likichangiwa na presha kutoka kwa mashabiki waliokuwa wakisubiri kwa hamu bao la ushindi uwanjani hapo. 

YANGA: Farouk Shikalo, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya/Tonombe Mukoko (dk75), Farid Mussa/Tuisila Kisinda (dk46), Feisal Salum ‘Fei Toto’, Michael Sarpong, Ditram Nchimbi na Deus Kaseke/Yocouba Sogne (dk46).

PRISONS: Jeremiah Kisubi, Michael Mpesa, Benjamin Asukile, Vedastus Mwihambi, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya/Kassim Mdoe (dk74), Lambert Sibiyanka, Mohamed Mkopi, Jeremiah Juma/Samson Mbagula (dk46) na Adilly Buha/Ezekeia Mwashilindi (dk50).

Katika michezo mingine ya ligi hiyo iliyochezwa mapema jana, Simba SC waliuanza msimu huu mpya kwa kishindo, wakiichapa Ihefu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, wakati Dodoma Jiji FC ikiitandika Mwadui bao, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mtibwa Sugar ililazimishwa suluhu na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa CCM Shabiby, uliopo Gairo, mkoani Morogoro, wakati Namungo FC iliichapa Coastal Union bao 1-0, Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi.

Kwa upande wao, Biashara United iliifunga Gwambina bao 1-0 kwenye Uwanja wa Karume, mjini Musoma, Mara.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa tatu, KMC ikiikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wakati Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa JKT Tanzania, Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, huku Azam FC wakikipiga na Polisi Tanzania, Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *