Posted By Posted On

BARBARA GONZALEZ,, on September 7, 2020 at 8:06 am

Mrithi wa Senzo Msimbazi, msomi aliyebebwa na Simba Dar MICHAEL MAURUS SIMBA imemteua Barbara Gonzalez kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya, akichukua mikoba iliyoachwa na Senzo Mbatha aliyejiuzulu nafasi hiyo na kutua Yanga. Senzo alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo Simba Agosti 9, mwaka huu na siku moja baadaye, alionekana na watu wa Yanga, ikielezwa alikuwa akisaini,

Mrithi wa Senzo Msimbazi, msomi aliyebebwa na Simba Dar

MICHAEL MAURUS

SIMBA imemteua Barbara Gonzalez kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya, akichukua mikoba iliyoachwa na Senzo Mbatha aliyejiuzulu nafasi hiyo na kutua Yanga.

Senzo alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo Simba Agosti 9, mwaka huu na siku moja baadaye, alionekana na watu wa Yanga, ikielezwa alikuwa akisaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani, Dar es Salaam.

Baadaye, uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Mshindo Msolla, ulimtangaza rasmi Senzo kama mshauri wa klabu hiyo.

Uteuzi wa Barbara, umefanywa na Bodi ya Wakurugenzi Simba chini ya Mwenyekiti wake, Mohammed Dewji ‘Mo’ katika kikao kilichofanyika Ijumaa ya wiki iliyopita jijini Dar es Salaam kabla ya kutangazwa juzi Jumamosi.

Mbali ya Mo Dewji, wajumbe wengine wa bodi hiyo walioshiriki katika utezu huo wa Barbara ni Salim Abdallah ‘Try Again’ (Makamu Mwenyekiti), Crescentius Magori, Zacharia Hanspoppe, Asha Baraka, Mulamu Ngh’ambi, Prof Mohammed Janabi na Mwina Kaduguda.

Wengine ni Octavian Mshiu, Kassim Dewji, Hussein Kitta (Mwanasheria), Ally Zawadi, Hassan Kipusi, Mulamu Nghambi, Mohamed Nassor, Musleh Rawah na Selemani Haroub.

Akimtambulisha Barbara baada ya uteuzi huo juzi, Mo Dewji alisema: “Hatujakurupuka kufanya maamuzi na wala sio maamuzi yangu, ni ya kikao kwani tulikaa jana (Ijumaa) na kuamua kumpitisha Barbara, anakuwa CEO wa kwanza mwanamke. Ni mchapakazi na anaipenda Simba, hivyo tunaamini kila kitu kitakwenda sawa.”

Kwa upande wake, Barbara alisema: “Mimi sio muongeaji sana ila ninawaahidi kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.”

Kama hiyo haitoshi, Barbara aliingia katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram na kutuma ujumbe uliosomeka: “Naishukuru Bodi ya Simba kwa kunipa heshima hii. Nitajitahidi kwa uwezo wangu wote kuitendea haki heshima hii.

“Kwa msaada wa Mungu na sapoti ya uongozi na mashabiki wa Simba, tutafikia malengo yetu ya kuifanya Simba kuwa klabu bora Afrika. Nawashukuru pia wote mlionipongeza.”

Hata kabla ya uteuzi huo, Barbara alishaonja ‘utamu’ wa nafasi hiyo alipopewa kuikaimu mara baada ya kujiuzulu kwa Senzo hivyo kujifunza mengi kuhusiana na soka na klabu ya Simba kwa ujumla.

Akizungumzia uteuzi wa Barbara, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Asha Baraka ‘Iron Lady’, alisema hawakukurupuka hata kidogo katika uamuzi huo.

Alisema kuwa kabla ya Barbara kupewa ‘shavu’ hilo, alikuwa majaribioni kwa kuratibu mchakato mzima wa tamasha la Wiki ya Simba na hatimaye kilele cha tukio hilo, maarufu kama Simba Day.

Alisema kuwa kutokana na jinsi alivyofanikiwa kufanikisha tamasha lao, wao kama bodi wakaona kuna kila sababu ya kumteua Barbara kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, wakiamini ana uwezo na sifa ya kuwafikisha pale wanapokusudia ambako si kwingine, bali kuifanya klabu yao kuwa tishio Afrika.

“Kuna watu wanadhani tumekurupuka katika uteuzi wa Barbara au ilikuwa ni bahari mbaya, nikuhakikishie Barbara ni mwanamke wa chuma, ana uwezo wa kuifanyia makubwa Simba. Kwa wasiofahamu, tulimpa jaribio la kuandaa shughuli nzima ya Simba Day na alifanikiwa kama sote tulivyojionea.

“Kwa watu waelewe kuwa Barbara yupo siku nyingi Simba, zaidi ya mwaka sasa anafanya kazi za Simba. Watu wanashtuka sasa hivi, sijui kwa kuwa ni mwanamke! Mwanamke pia ana uwezo wa kufanya kazi nzuri na kubwa tu.

“Sidhani kama wanachama wa Simba wana haja ya kuwa na hofu ya uteuzi wa Barbara uliofanywa na bodi, tupo wajumbe wa bodi walioteuliwa na Mo na tupo tuliochaguliwa na wanachama ambao tunalinda maslahi ya klabu. Hatujaona sehemu ambayo tumekosea, pale tutakapoona kuna jambo halipo sahihi, hatuwezi kukubali.

“Lakini pia ieleweke, Mo ameifanyia makubwa sana Simba na anaipenda sana Simba, kama kuna mwanachama ambaye kuna jambo haelewi, ni vema aulize, nasi tupo tutaliweka wazi, hakuna haja ya kuanza kurumbana wenyewe kwa wenyewe na kutoa mwanya kwa wapinzani wetu kutuvuruga.

“Naamini iwapo Barbara atapata ushirikiano wa kutoska kutoka kwa viongozi, mashabiki na wanachama, atatufikisha mbali,” alisema Asha ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (Aset), wamiliki wa bendi ya muziki ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, lakini pia akiwa ni bonge la mjasiliamali na mwanasimba ‘damu’.

UZOEFU WAKE KATIKA ONGOZI

Kabla ya kuukwaa ubosi Simba, Barbara alikuwa akihudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mo Dewji Foundation inayolenga kusaidia jamii mbalimbali, akiwa ameshiriki mipango kede kede ya kuikuza taasisi hiyo inayomilikiwa na Mohammed Dewji.

Lakini pia, Barbara amekuwa mshauri wa Bodi ya Young African Leaders Initiative (YALI)iliyozinduliwa na aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama kama ishara ya kusukuma mbele gurudumu la kizazi kipya kwenye uongozi barani Afrika  

Barbara pia ameitumikia Jumuiya ya Uongozi Afrika Mashariki na Kati, huku akiwa ameshawahi kuwa mshauri wa Taasisi ya Deloitte Consulting Limited Tanzania.

Kutokana na uwezo wake uliochangiwa na elimu, lakini pia kipaji cha uongozi, Barbara alishiriki katika miradi ya mbalimbali ya jamii pamoja na ile ya mashirika ya kimataifa kama USAID, UNICEF, Benki ya Dunia, Plan International, Shirika la VSO la London, Uingereza na mengineyo.

ELIMU

Barbara ni muhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Maendeleo aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Uchumi na Siasa jijini London, Uingereza pamoja na shahada ya Uchumi na Siasa aliyohitimu Chuo cha Manhattanville kilichopo mjini Purchase, New York, Marekani.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *