Posted By Posted On

Pete ya ndoa ya Ronaldo yazua gumzo, ‘imeua’ bil. 1.8/-

LONDON, England ACHANA na kila kitu juu ya takwimu zake za mabao, asisti au idadi ya mechi alizocheza akiwa na Manchester United, Real Madrid, Juventus au timu yake ya taifa ya Ureno. Gumzo kwa sasa ni kiasi cha fedha alichotumia Cristiano Ronaldo kumnunulia mpenzi wake pete ya uchumba, ikitajwa kuwa na thamani ya Pauni 615,000,

LONDON, England

ACHANA na kila kitu juu ya takwimu zake za mabao, asisti au idadi ya mechi alizocheza akiwa na Manchester United, Real Madrid, Juventus au timu yake ya taifa ya Ureno.

Gumzo kwa sasa ni kiasi cha fedha alichotumia Cristiano Ronaldo kumnunulia mpenzi wake pete ya uchumba, ikitajwa kuwa na thamani ya Pauni 615,000 (zaidi ya Sh bil. 1.8 za Tanzania).

Georgina Rodriguez, ambaye ndiye mrembo mwenyewe, anakuwa mwanamke aliyenunuliwa pete ya uchumba ya bei kali zaidi katika historia ya mchezo wa soka.

Kwa mujibu wa mtandao wa GamblingDeals, ambao umekusanya na kuanika bei za pete za uchumba zilizowahi kununuliwa na wanasoka, unaitaja hiyo ya ‘CR7’ kwa bibiye Georgina kuwa ndiyo funika bovu.

Ronaldo na Georgina wana mtoto wa kike mwenye umri wa miaka miwili, Alana, lakini mshikaji ana watatu ambao ni mapacha wenye miaka mitatu na kaka yao, Cristiano Jr (10).

Uhusiano wao ulianza mwishoni mwa mwaka 2016 na ilipofika mwaka juzi, Ronaldo alionekana kunogewa na ndipo alipomuomba binti huyo wa Kihispania wafunge ndoa.

Mara nyingi katika mahojiano yake, mpachikaji mabao huyo amekuwa akisisitiza kuwa wataona, kama alivyosisitiza mwaka jana alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV. “Amenisaidia sana na ukweli ulio wazi ni kwamba nampenda sana. Siku moja tutaoana kwa sababu pia ni ndoto ya mama yangu,” alisema.

Katika listi ya pete za ndoa za gharama kuwahi kununuliwa na wanasoka, inayofuata ni ile ya kipa wa timu ya taifa ya England, Jordan Pickford, aliyemnunulia mkewe wa sasa, Megan Davison, ikiwa na thamani ya Pauni 500,000 (zaidi ya Sh bil. 1.4 za Tanzania).

Nafasi ya tatu imeshikwa na pete aliyowahi kuinunua beki wa zamani wa Arsenal na Chelsea, Ashley Cole, ambayo ilimgharimu Pauni 275,000 kuinunua dukani na kumpelekea mkewe wa wakati huo, Cheryl.

Kyle Walker, beki wa Man City, yuko nyuma ya Cole, alipotumia Pauni 250,000 kununua pete ya ndoa kwa ajili ya mrembo wake, Annie Kilner, sawa na bei walizowahi kutumia Wayne Rooney, Rio Ferdinand na John Terry kwa wapenzi wao, Coleen, Kate Wright, na Toni.

Wakitoka hao, listi ina jina la Peter Crouch, ambaye alimuoa Abbey Clancy akiwa amemnunulia mlimbwende huyo pete yenye thamani ya Pauni 200,000.

Orodha inahitimishwa na Jack Wilshere na Harry Kane, ambao kila mmoja kwa wakati wake alitumia Pauni 180,000 (zaidi ya Sh mil. 530 za Tanzania) kununua pete aliyomvisha mpenzi wake. Wilshere alikuwa na bibiye Andriani Michael, wakati Kane na Katie Goodland.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *