Posted By Posted On

VIGOGO SIMBA WASHTUKA

NA ZAINAB IDDY BAADA ya sare ya bao 1-1 waliyoipata dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa juzi Jumamosi Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, vigogo wa klabu ya Simba, wamefanya kikao kizito na kuibuka na msimamo mkali. Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa mara baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa,

NA ZAINAB IDDY

BAADA ya sare ya bao 1-1 waliyoipata dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa juzi Jumamosi Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, vigogo wa klabu ya Simba, wamefanya kikao kizito na kuibuka na msimamo mkali.

Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa mara baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye kwa sasa hayupo nchini, aliwasiliana na viongozi wenzake na kufanya kikao kwa njia ya mtandao ili kujadili chanzo cha matokeo hayo na nini kifanyike.

Japo matokeo hayo yameonekana kuwaumiza mno viongozi wa timu hiyo, lakini mwisho wa siku wamekubaliana kutotafuta mchawi na badala yake, kujipanga upya.

“Ukweli ni kwamba matokeo yale hakuna aliyeyafurahia. Kutokana na kikosi chetu kilivyo, tunachotarajia ni ushindi wa mabao zaidi ya matatu na si sare.

“Hivyo, kuna mambo tumebaini ambayo si vema kuyaweka wazi, lakini msimamo wetu ni kwamba hatuhitaji tena matokeo kama ya Morogoro.

“Mo aliahidi kuzungumza na kocha (Sven Vandenbroeck) ili kufahamu tatizo, lakini zaidi kumpa msimamo wetu kama viongozi kwa niaba ya mashabiki na wanachama wa Simba,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.

Kiongozi huyo ambaye yupo ndani ya Bodi ya Simba, alisema wametuma ujumbe kwa wachezaji wakiwajulisha kuwa hawajafurahishwa na sare waliyopata Morogoro huku wakiwapa msimamo wao.

“Tumewataka wajitafakari, wafahamu kuwa Wanasimba wana matumaini makubwa sana kwao na wanawaamini wana uwezo wa kushinda mechi yoyote iwe ni nyumbani au ugenini.

“Tumewaambia tunataka kuona mechi ijayo, wanawafuta machozi mashabiki, kwani Wanasimba wanachohitaji kutoka kwa timu yao ni pointi tatu kila mechi na si sare wala kufungwa. Tunaamini watakuwa wametuelewa, hivyo tunasubiri mchezo ujao,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Swedy Mkwabi, amesema kutokana na kiwango kilichoonyeshwa Morogoro na timu yao, wana safari ndefu kutetea ubingwa wao wa ligi hiyo msimu huu.

Mkwabi ambaye alishuhudia mechi hiyo, aliliambia BINGWA jana: “Mechi ya kwanza licha ya kupata pointi tatu (dhidi ya Ihefu, Mbeya), lakini wachezaji wamekutana na upinzani mkubwa na hata hii ya jana (juzi), bado unaona ni jinsi gani timu pinzani zinaikamia Simba.

“Inawezekana ni kwa sababu Simba tayari ni mabingwa au wapinzania nao wanataka kuonyesha umwamba wao. Kwa hali hii, kama yatafanyika makosa kidogo tu ndani ya uwanja, nje au kwa uongozi, tutauweka rehani ubingwa wetu.

“Wachezaji wanapaswa kufahamu msimu huu wa ligi ni mgumu sana kwa Simba, hivyo wanatakiwa kujitoa katika hali zote ili waweze kuyafikia malengo  yaliyoweka, lakini pia hata uongozi unapaswa kutoruhusu aina yoyote ya mpasuko ili kutowachanganya vijana wetu.

“Simba ina nafasi kubwa ya kutetea taji la ubingwa msimu huu, kwa sababu wachezaji wengi wameendelea kuwa pamoja, lakini hiyo haitoshi kujihakikishia hilo, iwapo hakutakuwa na uchezaji wa jasho au damu kwa ajili ya timu.”

Naye Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, ameliambia BINGWA jana kuwa sababu ya kupata sare dhidi ya Mtibwa Sugar ni miundombinu mibovu waliyokutana nayo Uwanja wa Jamhuri.

“Yaweza kuonekana matokeo sio mazuri kwa kuwa tumepata sare, lakini kwetu hatuna mtazamo huo kwa sababu kupata alama nne ugenini katika viwanja kama vile, ni kitu cha kushukuru pia.

“Sasa tunarejea nyumbani kucheza na Biashara United, bila shaka utakuwa mchezo mzuri kwetu na ndio utakaotupa ushindi wa idadi kubwa ya mabao kulingana na uwanja tunaokwenda kuutumia,” alisema.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *