Posted By Posted On

MTAMKOMA… Morrison apelekwa kwa ‘babu’

NA MWANDISHI WETU KIWANGO kinachoonyeshwa na Bernard Morrison, kimewashtua watu wa Simba ambao wameamua kuingia msituni ili kurejesha makali yake. Akiwa Yanga, Morrison alikuwa ni moto wa kuotea mbali, akionyesha kiwango cha hali ya juu kilichowafanya Simba kufanya kila waliloweza na hatimaye kumtwaa kininja. Kati ya mambo yaliyowavutia Simba kwa Morrison, ni uwezo wake wa,

NA MWANDISHI WETU

KIWANGO kinachoonyeshwa na Bernard Morrison, kimewashtua watu wa Simba ambao wameamua kuingia msituni ili kurejesha makali yake.

Akiwa Yanga, Morrison alikuwa ni moto wa kuotea mbali, akionyesha kiwango cha hali ya juu kilichowafanya Simba kufanya kila waliloweza na hatimaye kumtwaa kininja.

Kati ya mambo yaliyowavutia Simba kwa Morrison, ni uwezo wake wa kiwango cha juu wa kumiliki mpira, chenga, uhodari wa kuwasumbua mabeki na kufunga mabao.

Lakini pia, Morrison alikuwa akiwapagawisha zaidi mabosi wa Simba kutokana na mtindo wake wa kutokimbia mabeki na zaidi anapopata mpira kuingia nao fasta eneo la hatari, utamaduni ambao hawana washambuliaji wengi hapa nchini.

Morrison alizidi kuwachochea mabosi wa Simba pale alipowafunga katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara Machi 8, mwaka huu ambao Yanga walishinda bao 1-0.

Nyota huyo kutoka Ghana, alifunga bao hilo pekee kwa mpira wa adhabu, mita takribani 23 kutoka golini baada ya kufanyiwa madhambi na kiungo wa Simba, Jonas Mkude.

Bao lile lilionekana kumpa umaarufu mkubwa Morrison, huku akikonga nyoyo za mashabiki wa Yanga ambao hawakuwa wakiamini kama timu yao inaweza kufurukuta mbele ya Simba yenye mastaa kibao.

Wakati watu wa Yanga wakiendelea kuchekelea bao la Morrison, wenzao wa Simba wakaanza kumfungia kazi mchezaji huyo na mwisho wa siku, wakafanikiwa kumpata kiulaani.

Lakini tangu ameanza kuichezea Simba, Morrison ameshindwa kuonyesha kile ambacho Wekundu wa Msimbazi walikitarajia kutoka kwake.

Ukiachana na mechi ya kirafiki ya Simba Day dhidi ya Vital’O ya Burundi ambayo aling’ara, mechi mbili za ligi alizocheza dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar, hakuwa na maajabu.

Kwa kufahamu hilo, kuna watu wa Simba wameamua kumsaidia mchezaji huyo kwa kupanga kumpeleka kwa wazee wa klabu hiyo ili kusomewa dua aweze kurejea katika kiwango chake.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa kuna mmoja wa wazee wa klabu hiyo amejitolea kumsomea Morrison dua ili kumwondolea mikosi yote aweze kuwapa raha Wanamsimbazi.

“Tunadhani kuna kitu, Morrison wa Yanga sio huyu tunayemuona Simba. Wapo wanaosema labda kwa kuwa alichezea viwanja vya ugenini ambavyo si vizuri, lakini mbona alionyesha kiwango kizuri akiwa Yanga walipocheza na Mwadui na mechi nyingine za mikoani?

“Kuna mzee amejitolea kumpeleka kwa wazee wenzake wakamsomee dua ili kuondoa mikosi na nuksi zote alizonazo, huenda ndiizo zinazochangia kushuka kwa kiwango chake,” alisema mtoa habari wetu ambaye hakupenda jina lake liwekwe wazi.

Alisema kuwa wamefanya kufanya hivyo bila kumshirikisha kiongozi yeyote wa Simba kwani wanaweza kuzia mpango huo.

Mapema jana, kulizuka habari zilizosema kuwa Morrion ameomba kuondoka Simba ili arejee kwao Ghana ‘kujipanga’ zaidi, kwani hafurahishwi na kiwango chake cha sasa uwanjani.

BINGWA liliwatafuta viongozi wa Simba jana kufahamu kama kuna ukweli juu ya hilo, lakini simu zao muda mwingi zilikuwa zikitumika hadi gazeti hili linakwenda mitamboni.

Lakini mmoja wa watu wa benchi la ufundi la Simba, ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi, alisema: “Hakuna kitu kama hicho, Morrison hakuomba ruhusa na hivi ninavyozungumza na wewe yupo na wenzake na ni miongoni mwa watakaocheza mechi yetu ya ligi ya mwishoni mwa wiki.”

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *