Posted By Posted On

KISHINDO SIMBA SC

MWANDISHI WETU WIKIENDI hii inaweza kuwa ya aina yake kwa wapenzi wa Simba kutokana na mikakati inayosukwa na viongozi wao, kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. Mchezo huo ni wa kwanza kwa Simba kwenye uwanja wao huo wa nyumbani, baada ya,

MWANDISHI WETU

WIKIENDI hii inaweza kuwa ya aina yake kwa wapenzi wa Simba kutokana na mikakati inayosukwa na viongozi wao, kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni wa kwanza kwa Simba kwenye uwanja wao huo wa nyumbani, baada ya kukipiga ugenini mara mbili na kuambulia poiti nne kati ya sita.

Simba ilianza kukata utepe wa ligi hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kwa kuvaana na Ihefu kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na kushinda mabao 2-1.

Baada ya hapo, Wekundu wa Msimbazi hao, waliwafuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na kuambulia sare ya bao 1-1.

Japo pointi nne za ugenini si haba, lakini zimeonekana kutowafurahisha wapenzi wa Simba ambao wanaamini kutokana na ubora wa kikosi chao, hawakustahili kupoteza pointi yoyote.

Wapo wanaofika mbali zaidi kwa kudhani hata Ihefu ambayo imepanda daraja msimu huu, ilistahili kufungwa mabao zaidi ya matano na si ushindi wa 2-1 walioupata, tena wakiwa na kikosi kilichosajiliwa kwa mamilioni ya fedha tofauti na ilivyo kwa wageni hao wa Ligi Kuu Bara.

Ni kutokana na manung’uniko hayo ya baadhi ya wapenzi wa Simba, akiwamo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’, viongozi wa juu wa Wekundu wa Msimbazi hao, waliamua kufanya vikao kuona ni vipi kikosi chao kinakata kiu ya Wanasimba, yaani kupata ushindi mnono.

Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa jana Ofisa Mtendaji Mkuu (C.E.O) wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, alikutana na viongozi wenzake kujadili mambo kadha wa kadha, zaidi ikiwa ni jinsi ya kuthibitisha ubora wa kikosi chao kesho na katika mechi zinazofuata.

“Leo (jana) toka asubuhi, mabosi walikuwa na kikao kizito, wakiongozwa na C.E.O Barbara. Inavyoonekana bado hawajafurahishwa na matokeo tunayopata, hivyo wanaweka mikakati ya kuhakikisha timu inashinda mabao mengi zaidi ili kuwaridhisha mashabiki.

“Unajua mashabiki wa Simba wanaamini timu yao ni bora kuliko timu yoyote hapa nchini, hivyo inapotoka sare na timu kama Mtibwa au kuifunga Ihefu mabao 2-1, wanapatwa na ukakasi na kuanza kujiuliza kulikoni. Wao wanataka wakicheza na timu kama Ihefu, washinde mabao hata saba wakiamini kikosi chao ni bora zaidi ya timu zote za Ligi Kuu.

“Sasa kinachoonekana, viongozi wameliona hilo, hivyo wamekuwa wakikutana wiki yote hii kujadiliana hilo, lakini pia wakiwashirikisha makocha na hata baadhi ya wachezaji, hasa wale mastaa kuona nini tatizo na vipi wanaweza kukata kiu ya mashabiki.

“Viongozi wanahofia iwapo timu itaendelea na matokeo yasiyoridhisha, wanaweza kuwakatisha tamaa mashabiki na kupotea viwanjani,” alisema mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.

Ili kuthibitisha ukweli wa maelezo hayo ya kiongozi huyo, BINGWA jana mchana lilipiga hodi ofisini kwa CEO wa Simba, Barbara na kujulishwa kuwa aliondoka toka asubuhi, ikielezwa alikuwa kikaoni.

Bosi huyo wa Msimbazi alipopigiwa simu, aliikata na kuomba kutumiwa ujumbe kwani alikuwa katika kikao kizito na viongozi wenzake.

Habari zilizopatikana jana jioni wakati gazeti hili likielekea mitamboni, zinasema kuwa kikao hicho kimeibuka na maazimio mazito, yanayolenga kuwapa raha wapenzi wa klabu hiyo kuanzia kesho watakapoivaa Biashara United ya mkoani Mara.

“Kilikuwa kikao cha kawaida tu kama ilivyo kwa vingine. Inafahamika kuwa Jumapili (kesho) tuna mechi na Biashara, hivyo tulikuwa tukiweka mikakati kadhaa ya kuona ni namna gani timu yetu inawapa raha mashabiki wa Simba.

“Kuna mipango mingi tuliyopanga ambayo si sahihi kuianika kwenye vyombo vya habari. Ninachoweza kusema, wapenzi wa Simba wajitokeze kwa wingi uwanjani Jumapili ili kupata raha kutoka kwa wachezaji wao.

“Kocha ametuhakikishia burudani na ushindi mnono katika mchezo huo ambao ni mhimu sana kwetu,” alisema mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba alipozungumza na BINGWA jana jioni. 

Kutokana na mikakati inayosukwa na viongozi hao wa Simba, ni wazi Biashara United wakizubaa tu kesho, wanaweza kujikuta wakipokea kipigo cha ‘mbwa mwizi’ na mwisho wa siku, kupoteana na hata kusahau basi lililowapeleka Uwanja wa Mkapa, uliopo wilayani Temeka, Dar es Salaam.

Ikumbukwe kuwa mapema wiki hii, Barbara alikutana na Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck ofisini kwake, Dar es Salaam ili kuteta naye, zaidi ikiwa ni kupata mrejesho wa mechi zao mbili za mikoani dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar, lakini pia kusuka mipango ya mechi zijazo.

Pia, bosi huyo wa Simba alikutana na mmoja wa nyota wao, Bernard Morrison ofisini kwake kama sehemu ya mikakati yake ya kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake ndani ya timu yao.

Akiwa kama mtendaji mkuu wa klabu ya Simba, Barbara aliyekabidhiwa nafasi hiyo hivi karibuni, ameamua kuchukua hatua kadhaa ili kuhakikisha Wanasimba wanaendelea kupata raha kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Katika mahojiano na BINGWA katikati ya wiki iliyopita, Barbara alisema kuwa amepanga kuweka utaratibu ambao utaiwezesha kila idara ya klabu hiyo, likiwamo benchi la ufundi na hata wachezaji, kutimiza majumu yake.

Pia, aliahidi kuipa darasa Idara ya Habari na Mawasiliano iliyopo chini ya Haji Manara ili iweze kutimiza majukumu yake kulingana na mahitaji ya klabu na Wanasimba kwa ujumla.

“Nitakutana na kila idara kuona ni vipi tunafanya kazi kwa weledi, huku tukiweka mbele maslahi ya klabu na si ya mtu binafsi. Simba ni taasisi kubwa yenye mamilioni ya mashabiki nyuma yake, hivyo siwezi kukubali kuona mambo yanakwenda ovyo na kuwanyima raha Wanasimba,” alisema Barbara alipozungumza na BINGWA wiki iliyopita.      

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *