Posted By Posted On

NI PASI, MABAO

NA WINFRIDA MTOI KIKOSI cha Tanga leo kinashuka kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, kuvaana na wenyeji wao, Kagera Sugar, huku Wanajangwani hao wakiahidi kutoa burudani ya aina yake kwa wapenzi wao. Burudani hiyo itatokana na soka maridadi la pasi za uhakika na mabao ya kutosha ambayo mwisho wa siku, yatawawezesha kutoka uwanjani na ushindi,

NA WINFRIDA MTOI

KIKOSI cha Tanga leo kinashuka kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, kuvaana na wenyeji wao, Kagera Sugar, huku Wanajangwani hao wakiahidi kutoa burudani ya aina yake kwa wapenzi wao.

Burudani hiyo itatokana na soka maridadi la pasi za uhakika na mabao ya kutosha ambayo mwisho wa siku, yatawawezesha kutoka uwanjani na ushindi mnono.

Wanajangwani hao wataivaa Kagera Sugar katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakiwa wametoka kukusanya pointi nne nyumbani, wakishinda mechi moja na kupata sare moja kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hizo, ilitoka sare ya 1-1 na Tanzania Prisons kabla ya kuifunga Mbeya City bao 1-0.

Mchezo dhidi ya Kagera, utakuwa wa kwanza kwa Yanga, nje ya Dar es Salam tangu ligi hiyo ilipoanza Septemba 6, mwaka huu na sasa ikiwa ni raundi ya tatu.

Baada ya mchezo wa leo, Yanga itawafuata Mtibwa Sugar ya mjini Morogoro wikiendi ya wiki ijayo.

Kutokana na ushindi waliopata dhidi ya Mbeya City, mechi ya leo itaangaliwa zaidi, kila Mwanayanga na wadau wengine wa soka wakitaka kufahamu nini kikosi hicho kitafanya kikiwa ugenini.

Mara ya mwisho Yanga kukutana na Kagera  kwenye uwanja huo, iliibuka na ushindi wa  bao 1-0, lakini mchezo wa kwanza uliopigwa Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-0.

Wanayanga wengi hasa wa mikoa ya jirani na Kagera, wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kuona vitu vya nyota wao wapya, hasusan Carlos Carlinhos aliyeanza kuwa gumzo.

Carlinhos raia wa Angola ambaye amefunika hata katika mapokezi yake, vitu alivyovifanya katika mechi dhidi ya Mbeya City, vimemfanya kuwa Mfalme wa Jangwani.

Moja ya kitu kinachowavutia mashabiki wengi wa Yanga kwa kiungo huyo, ni aina ya pasi anazopiga anapokuwa uwanjani, pamoja na kona aliyochonga dhidi ya Mbeya City na kuzaa bao lililoipa ushindi timu yake.

Ukiachana na Carlinhos, burundani nyingine ipo kwa nyota wawili kutoka DR Congo, Tonombe Mukoko na Tuisila Kisinda, huku mwingine akiwa ni straika Mghana, Michael Sarpong.

Katika kudhihirisha kuwa mashabiki wa Yanga mkoani humo wamepania kuona burudani, ni mapokezi waliyofanya wakati nyota hao wanawasili Bukoba juzi.

Kingine kinachowapa jeuri Yanga, ni Uwanja wa Kaitaba kuwa mzuri tofauti na vingine vya mikoani kwani umejengwa na nyasi bandia kama walizotoka kutumia katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mlandege, Azam Complex.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, ameliambia BINGWA kuwa wamejipanga vizuri, hivyo hakuna cha kupoteza, akiwaita mashabiki wote wa Kanda ya Ziwa kutua Bukoba ili kuungana na wenzao wa huko kuvunja rekodi ya kuujaza Uwanja wa Kaitaba.

“Timu imefanya mazoezi ya mwisho vizuri, hakuna majeruhi, wachezaji wote wako fiti, nawaomba Wanayanga wote kama walivyotupokea, wafike uwanjani kuendelea kutusapoti hadi dakika ya mwisho,” alisema Saleh.

Naye Mkuu wa msafara huo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema kuna kitu kikubwa watakifanya mkoani humo.

“Tumekuja Kagera kusaka ushindi na kutoa  burudani kuwafurahisha Wanayanga, kuna kitu kikubwa kitafanyika Jumamosi (leo), kikosi hiki ni tofauti na vile walivyozoea,” alisema.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *