Posted By Posted On

KISASI, Zaha anapoitungua United kwa hasira za mrembo Lauren Moyes

MANCHESTER, England JUZI ilikuwa siku mbaya kwa Mashetani Wekundu baada ya kudondosha pointi zote tatu mbele ya Crystal Palace, mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa katika Uwanja wa Old Trafford. Aidha, kupoteza pointi tatu wala si ishu kubwa, bali kichapo cha mabao 3-1 ndicho kilichowashangaza wengi, tena Man United ikiwa nyumbani! Kwa upande mwingine, mashabiki wa,

MANCHESTER, England

JUZI ilikuwa siku mbaya kwa Mashetani Wekundu baada ya kudondosha pointi zote tatu mbele ya Crystal Palace, mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa katika Uwanja wa Old Trafford.

Aidha, kupoteza pointi tatu wala si ishu kubwa, bali kichapo cha mabao 3-1 ndicho kilichowashangaza wengi, tena Man United ikiwa nyumbani!

Kwa upande mwingine, mashabiki wa Man United wataendelea kulia na Winfred Zaha kwani ndiye aliyezitikisa mara mbili nyavu zao katika mchezo huo.

Wakati huo huo, hakuna asiyefahamu kuwa Zaha raia wa Ivory Coast ni kama amewaadhibu wabaya wake, ikikumbukwa kuwa aliwahi kusugua benchi akiwa mchezaji wa Man United.

Zaha alitua Old Trafford mwaka 2013. akiwa ni mchezaji wa mwisho kusajiliwa na kocha Alex Ferguson, wakati huo Man United wakimnasa kwa Pauni milioni 10. 

Lakini, Zaha alijikuta akiishia benchi chini ya kocha aliyefuata, David Moyes, hivyo akapelekwa kwa mkopo Cardif City, kabla ya kuuzwa kabisa katika klabu yake ya zamani, Palace.

Aidha, unapozungumzia kukwama kwa Zaha akiwa Man United, hutaacha kumtaja mrembo aitwaye Lauren, binti wa aliyekuwa kocha wa timu hiyo wakati huo, David Moyes.

Hakuna aliyekuwa anapingana na uwezo wa Zaha katika upachikaji mabao lakini Lauren ndiye aliyemponza na kuishia kuwa mchezaji wa akiba kila Moyes alipopanga kikosi.

Kile kilichoelezwa kumkera Moyes na kumpotezea mazima Zaha ni taarifa zilizoibuliwa na kituo cha televisheni cha Sky Sport zikidai nyota huyo aliyekuwa na umri wa miaka 19 kipindi hicho, ana uhusiano wa kimapenzi na Lauren.

Kabla ya mechi kati ya Man United na Palace usiku wa juzi, Patrice Evra aliyekuwa beki tegemeo wakati Zaha akiwa Man United, alisema:

“Nafikiri kilichoharibu maisha yake ya soka ndani ya Manchester United ni kuwapo kwa taarifa hizo za kutoka kimapenzi na binti wa David Moyes,” alisema aliyekuwa staa wa Man United kipindi hicho, Patrice Evra.

“Kwa sababu nakumbuka alikuwa kwenye kiwango kizuri sana tukiwa kwenye maandalizi ya msimu lakini zilipoibuka taarifa hizo, akawa hachezeshwi na akapotea kabisa.”

Kipindi chote hicho, Zaha aliendelea kusisitiza kuwa si tu ni uongo kwamba alikutwa kitandani na Lauren, bali pia hajawahi kumuona kabisa msichana huyo anayezungumziwa.

Hivi karibuni, Zaha aliibuka tena akisema anawalaani mabosi wa Man United kwa kuwa hakuna aliyesimama upande wake kujaribu kumsafisha kutokana na skendo hiyo.

“Kulikuwa na tetesi kuwa sichezeshwi kwa sababu nililala na mtoto wa kocha, David Moyes. Hakuna hata mmoja pale klabuni aliyenipigania kuondosha uzushi huo,” alisema na kusisitiza: “Ni kama nilikuwa napigana mwenyewe juu ya taarifa hizo nilizojua kabisa kuwa ni uzushi.”

Akasema ni kweli akiwa Man United alikuwa akiingiza mkwanja wa maana lakini uzushi uliokuwa ukiendelea juu yake ulimfanya akose raha ya kuishi jijini Manchester.

Juzi, ikiwa ni miaka saba imepita, kituo cha runinga cha Sky Sports kililazimika kuomba radhi kwa kile kilichodai kilipotosha kwa taarifa yake ya Zaha kutoka kimapenzi na binti wa Moyes.

Alikuwa ni mtangazaji wake, Kelly Cates, ndiye aliyebeba mzigo wa kuomba radhi, akisema ni taarifa zisizo na uhakika, hivyo zinapaswa kupotezewa.

“Tunalazimika kuweka sawa kile tulichowahi kusema katika vipindi vyetu, kwamba kulikuwa na uhusiano kati ya Wilfried Zaha na binti wa David Moyes. Tunaelewa kabisa kuwa Wilfried Zaha hakuwahi kukutana na binti wa David Moyes…” alisema Cates.

Zaha amekuwa moto wa kuotea mbali kwa mabeki na walinda mlango Ligi Kuu ya England tangu alipoondoka Old Trafford mwaka 2014 akiwa amecheza mechi nne tu katika msimu wake wa kwanza.

Huku klabu kubwa zikiimendea saini yake kila kinapofika kipindi cha usajili, mchezaji huyo ni tegemeo kwenye kikosi cha Palace akiwa amecheza mechi zaidi ya 360.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *