Posted By Posted On

Nyota Yanga mtegoni

ZAINAB IDDY LICHA ya kocha, Zlatko Krmpotic, kuiongoza Yanga kupata pointi saba katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara waliyocheza hadi sasa, lakini ukweli ni kwamba bado ana mtihani mzito wa kusaka kikosi cha kwanza. Kocha huyo raia wa Serbia, amekuwa akitumia wachezaji tofauti katika kikosi chake cha kwanza katika michezo yote mitatu iliyochezwa,

ZAINAB IDDY

LICHA ya kocha, Zlatko Krmpotic, kuiongoza Yanga kupata pointi saba katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara waliyocheza hadi sasa, lakini ukweli ni kwamba bado ana mtihani mzito wa kusaka kikosi cha kwanza.

Kocha huyo raia wa Serbia, amekuwa akitumia wachezaji tofauti katika kikosi chake cha kwanza katika michezo yote mitatu iliyochezwa nyumbani na ugenini.

Mchezo wa kwanza dhidi ya Tanzania Prisons alianza na kundi kubwa la wachezaji wazawa na wageni wawili tu, ambapo kipindi cha kwanza hawakucheza vizuri hadi alipofanya mabadiliko.

Mchezo uliofuata alianzisha wachezaji wengi waliocheza kipindi cha pili katika mchezo dhidi ya Prisons na kufanikiwa kuvuna pointi tatu dhidi ya Mbeya City ndani ya Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Prisons.

Lakini sasa kocha huyo amepanga kutumia mechi tano zijazo kusaka kikosi cha kwanza, ambacho hakitakuwa na mabadiliko ya mara kwa mara kama ilivyotokea kwenye michezo iliyopita ya ligi hiyo.

Hatua hiyo,  itaibuka vita kwa wachezaji wake kwani kila mmoja atalazimika kuonesha juhudi mazoezini ili kupenya kikosini.

Katika kufanikisha hilo, tayari Yanga imecheza michezo mitatu ya Ligi Kuu na miwili tu,  imesalia kabla uamuzi mgumu haujatolewa na kocha huyo raia wa Serbia.

 BINGWA limepenyezewa  habari jana, zinasema Zlatko alitoa michezo hiyo mitano kwa wachezaji  baada ya kumalizika  ule dhidi ya Mbeya City uliofanyikwa Septemba 7,mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa.

“Tumeshacheza mechi tatu sasa zimesalia mbili tu, jana baada ya kupata chakula cha jioni na wanachama wa Yanga kule Kagera, kocha aliwakumbusha wachezaji kuwa mpango wake wa kuchuja kikosi unaendelea na imebaki michezo hiyo. 

“Hili halitokuwa na mjadala, uongozi wa juu tumebariki mpango huu wa benchi la ufundi, lakini pia ikitokea mchezaji amebahatika kuingia katika kikosi cha kwanza akishuka kiwango hatokwenda kwa wanaoanzia benchi bali atapelekwa kwa wale wa jukwaani.

 “Tumekubaliana na mpango huo wa benchi la ufundi baada ya kuona utasaidia kuwa na wachezaji wanaojituma muda wote hasa ukizingatia bonasi zitakuwa zinatolewa kwa wale wanaocheza tu, hivyo wale wa jukwaani au wanaoanzia benchi wasitegemee kuwa sawa na aliyeanza mchezo na kuitumikia kwa zaidi ya dakika 60 za mchezo.” Alisema mtoa habari wetu.

Kutokana na hilo, Yanga imesalia michezo miwili itakayoamua hatima ya wachezaji ambao wataunda kikosi cha kwanza cha Wanajangwani hao, ikiwamo dhidi ya Mtibwa Sugar  utakaochezwa wikiendi kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, kisha watarejea Dar es Salaam kupepetana na Polisi Tanzania, kwenye Uwanja wa Mkapa. 

Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kimewasili jijini Dar es Salaam jana asubuhi kikitokea mkoani Kagera na wachezaji kupewa mapumziko ya siku moja kabla ya kuanza maandalizi ya kuwakabiji Mtibwa Sugar.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *