Posted By Posted On

WACHEZAJI WA KIGENI WAING’ARISHA YANGA LIGI KUU

Msomaji wa Yanganews Blog:Kikosi cha Yanga imecheza mechi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa imeshinda michezo miwili na kutoka sare moja, ikicheza mechi mbili nyumbani na nyingine ugenini.

Mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu, Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikaifunga Mbeya City kwenye uwanja huo huo, kabla ya Jumamosi iliyopita kushinda kwa mara ya kwanza ugenini bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Imejikusanyia pointi saba, magoli matatu, ikiwa imefungwa bao moja.

Ukiangalia timu hiyo mpaka kufikia raundi ya tatu imebebwa zaidi na wachezaji wa kigeni zaidi.

Ni wale iliyowasajili msimu huu na wale waliokuwapo awali.

Mpaka sasa ambapo Yanga ina magoli matatu, yote yamefungwa na wachezaji wa kigeni, huku kukiwa hakuna mchezaji yoyote wa Kitanzania aliyefunga goli kwenye timu hiyo.

MICHAEL SARPONG (Yanga 1-1 Prisons)

Huyu ni raia wa Ghana na ndiye mchezaji wa kwanza wa Yanga kufunga msimu huu kwenye Ligi Kuu.

Alifanya hivyo dakika ya 18 kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons. Wakati huo tayari Prisons ilikuwa imeshapata bao moja kupitia kwa Lambart Subianka.

Ilitokea hekaheka kwenye lango la Prisons, kutokana na mpira uliokokotwa na Farid Mussa, alipiga krosi iliyookolewa vibaya na mabeki wa Prisons.

Sarpong, straika aliyesajiliwa msimu huu akitokea Rayon Sport ya Rwanda, aliukuta mpira ukiwa unazagaazagaa akaujaza wavuni na mechi hiyo ikaisha kwa sare ya bao 1-1, akawa ameiokoa Yanga na kipigo.

Mechi hiyo ilichezwa Septemba 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

LAMINE MORO (Yanga 1-0 Mbeya City)

Beki wa kati, Lamine Moro aliipatia Yanga bao pekee kwenye mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Septemba 13, mwaka huu.

Lamine pia ni raia wa Ghana, akiwa mmoja wa wachezaji wa kigeni walioing’arisha Yanga kwenye mechi za Ligi Kuu mpaka sasa.

Ilikuwa ni dakika ya 85, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Yanga wakiwa wameshaanza kutoka uwanjani wakiwahi usafiri, wengine kwenye magari yao binafsi, kila mmoja akidhani mechi ingeenda sare, mambo yalibadilika.

Ilikuwa ni kona wa mchezaji mwingine mpya wa kigeni, Carlos Carlinhos kutoka Angola, iliyokwenda kutua kwenye kichwa cha mchezaji huyo wa kigeni ambaye yupo kwa msimu wa pili sasa, Lamine akaukwamisha wavuni.

Ni bao lililowafanya Yanga kutoka uwanjani na ushindi wa bao 1-0, ikipata pointi tatu na kuifanya kuongeza na kufikia ponti nne.

MUKOKO TONOMBE (Yanga 1-0 Kagera Sugar)

Ni mechi juzi Jumamosi ambayo mchezaji mwingine wa kigeni, Mukoko Tonombe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), aliifungia Yanga bao dakika ya 72 na kuifanya timu hiyo kutoka uwanjani na ushindi wa bao 1-0, kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Ni mechi ya kwanza kushinda ikiwa ugenini. Mukoko alifunga bao hilo pekee akipata pasi maridadi kutoka kwa Mkongomani mwenzake, Tuisila Kisinda ambaye alimtambuka, Ally Sonso wa Kagera Sugar kwenye winga ya kulia, akaingia ndani na kutoa pasi kwa mfungaji ambaye aliugusa mara ya kwanza, kabla ya kuachia shuti la juu lililojaa wavuni na kushinda kipa Ramadhani Chalamanda.

,,Read More

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *