Posted By Posted On

CHAMA GUMZO KILA KONA

NA WINFRIDA MTOI KIWANGO kilichoonyeshwa na kiungo wa Simba, Clatous Chama katika mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United, kimeendelea kuwa gumzo kila kona, huku akipewa nafasi ya kutetea tuzo yake ya mchezaji bora msimu huu. Sambamba na hilo, uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mohammed,

NA WINFRIDA MTOI

KIWANGO kilichoonyeshwa na kiungo wa Simba, Clatous Chama katika mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United, kimeendelea kuwa gumzo kila kona, huku akipewa nafasi ya kutetea tuzo yake ya mchezaji bora msimu huu.

Sambamba na hilo, uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mohammed Dewji ‘Mo’ na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, wamepewa jukumu la kushughulikia mkataba wa Mzambia huyo utakaomalizika Juni mwakani.

Katika mchezo huo wa juzi uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Simba ilishinda mabao 4-0, huku Chama akitupia mara mbili.

Mbali ya kufunga, Chama alitoa pasi maridadi ya bao (assist) kwa kisigino iliyomkuta Chriss Mugalu na kucheka na nyavu, kuifungia Simba bao la nne.

Kwa ujumla, Chama aling’ara vilivyo katika mchezo huo, huku bao lake la pili akilifunga kwa ustadi wa hali ya juu.

Baada ya mchezo huo, jina la Chama lilianza kuteka hisia za mashabiki wa Simba, wakimpachika kila aina ya jina waliloona linalingana na uchezaji wake siku hiyo.

Katika mitandao ya kijamii, wapenzi wa Simba walituma video za bao lake la pili na pasi ya bao lililofungwa na Mugalu aliyotoa kwa kisigino, huku Mzambia huyo akipewa kila aina ya sifa.

Akimzungumzia Chama, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, alisema kuwa amefurahishwa na kiwango chake, kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine.

“Hata hivyo, furaha yangu ni hiki tulichokipata, tumeshinda ushindi mkubwa na bila kuruhusu bao na tumekaa katika nafasi ya pili,” alisema Sven.

Alisisitiza: “Ninachofahamu Chama anamaliza mkataba Juni mwakani, lakini suala hilo linauhusu uongozi kuona ni vipi wanashughulikia mkataba wake pamoja na mchezaji mwenyewe.”

Sven alisema kuwa kikosi chake kwa sasa kinaweza kucheza vyovyote anavyotaka kwa kuwa kila mchezaji anaweza kufunga na kutoa pasi ya bao.

Alisema  hana wasiwasi juu ya upangaji wa kikosi chake, akifanya hivyo kulingana na mazoezi waliyofanya au aina ya mchezo.

Alisema kikosi alichopanga juzi, alikuwa akifahamu mbinu watakayokuja nayo Biashara United, kuweka walinzi wengi kuwadhibiti hali iliyomfanya ajipange na mbinu mbalimbali.

Alisema kuwa kingine anachokiangalia wakati anapanga kikosi chake ni uwanja wanaotumia na timu wanayotarajia kukutana nayo.

“Kwa wachezaji nilionao na mazoezi tuliyofanya katika maandalizi, yeyote anaweza kufunga au kutoa pasi ya bao (assist).

“Naweza nikaamua leo nichezeshe straika mmoja, wawili, watatu na hata siku nyingine nikiamua nisiweke, inategemea na mbinu tunayotaka kutumia,” alisema Sven.

Alitolea mfano Mzamiru Yassin kuwa si straika, lakini kwa sasa ana mabao mawili na ‘assist’ moja katika mechi tatu walizocheza, hiyo inaonyesha nguvu kubwa iliyopo kwenye timu.

Sven alisema kwa ujumla ameridhishwa na kiwango walichocheza nyota wake wote, walioanza na kuingia baadaye, kila mmoja alikuwa anajituma.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Biashara United, Francis Baraza, amekiri kuwa amekutana na timu bora na amekubali kilichotokea.

“Siwezi kumlaumu mchezaji yeyote, mipango yangu ilikuwa ni kupata sare, imeshindikana, tunakwenda kujipanga na mchezo ujao,” alisema Baraza.

Mbali ya mabao mawili ya Chama na lile la Mugalu, lingine la Simba lilifungwa na Meddie Kagere.

Simba ilianza ligi kwa kuichapa Ihefu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, kabla ya kutoka sare ya nao 1-1 na Mtibwa Sugar, Dimba la Jamhuri, Morogoro.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *