Posted By Posted On

MHILU AIPAA USHINDI WA KWANZA KAGERA SUGAR LIGI KUU, NAMUNGO NAYO YAIPIGA 1-0 MBEYA CITY

Na Mwandishi Wetu, BUKOBA

TIMU ya Kagera Sugar imepata ushindi wa kwanza wa msimu baada ya kuichapa KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam 1-0 leo Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Pongezi kwa kiungo mshambuliaji Yussuf Mhilu aliyerejea uwanjani leo baada ya kuwa nje tangu mwanzo kutokana na maumivu – ambaye leo amefunga bao hilo pekee dakika ya 33.

Sasa Kagera Sugar inafikisha pointi nne baada ya kucheza mechi nne, tatu za awali ikifungwa mbili 1-0 zote na JKT Tanzania na Yanga hapo hapo Kaitaba na nyingine ikitoa sare ya 0-0 na Gwambina huko Misungwi, mkoani Mwanza.

Yussuf Mhilu akishangilia baada ya kuifungia bao pekee Kagera Sugar ikiichapa KMC 1-0 leo Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba 

Mechi nyingine ya leo, bao pekee la Bigirimana Blaise dakika ya 10 limeipa Namungo FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mbeya City Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya leo.

Namungo inafikisha pointi sita baada ya kucheza mechi nne, ikishinda mbili na kufungwa mbili – wakati Mbeya City hali inazidi kuwa mbaya, kwani inabaki bila pointi kutokana na kufungwa mechi zote nne hadi sasa na inashika mkia 

Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu; Tanzania Prisons ikiwakaribisha Azam FC Uwanja wa Nelson Mandela huko Sumbawanga mkoani Rukwa, Polisi Tanzania na Dodoma Jiji Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na Simba SC na Gwambina Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Jumapili Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Biashara United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Mwadui FC na Ihefu Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga na Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Raundi ya Nne ya Ligi Kuu itakamilishwa Jumatatu kwa mchezo mmoja tu, Coastal Union wakiwa wenyeji wa JKT Tanzania kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *