Posted By Posted On

KIBWANA WALA HANA HOFU, USHINDANI WA NAMBA YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Beki wa mabingwa wa kihistoria Yanga,Kibwana amecheza mechi zote tatu za Ligi Kuu msimu huu na amekuwa akianza kikosi cha kwanza lakini kupona kwa beki mwenzake Paul Godfrey ‘Boxer’ kutamfanya apambane zaidi kujihakikishia haondolewi kikosi cha kwanza.

Katika mechi mbili ambazo Yanga wamecheza dhidi ya Prisons na Mbeya City, Kibwana alicheza dakika zote 90 wakati mechi na Kagera Sugar alifanyiwa mabadiliko kipindi cha pili na aliingia Deus Kaseke ambaye kiasili ni winga.

Kibwana amesema ni changamoto kubwa kuwa na wachezaji wengi wanaocheza eneo lake lakini hilo halimpi shida kwani anaamini kiwango chake ni kikubwa.

“Timu ina wachezaji wengi na wote wana uwezo mkubwa hivyo kocha ndiye ataamua ampange nani na kwa mechi gani, binafsi naamini nina uwezo wa kupata nafasi na kuisaidia timu kufikia malengo yake ambayo ni kupata ushindi kwa kila mechi,” alisema Kibwana.

Pia beki huyo mwenye umri wa miaka 20, amewatuliza mashabiki wa Yanga kwa kuwataka kuwa wavumilivu pale timu inapopata matokeo yoyote.

“Tuna timu nzuri na tunacheza kwa mfumo elekezi kutoka kwa makocha, mashabiki wanapaswa kuwa wavumilivu na kutuamini vijana wao tunapokuwa uwanjani kwani tunatambua wanataka ushindi, tupo pale kwa ajili ya kutafuta ushindi ili tusonge mbele na wao wafurahie kuipenda Yanga,” alisema Kibwana

Yanga wamemsajili Kibwana ambaye msimu uliopita aliichezea Mtibwa Sugar ambayo ndiyo timu iliyomlea kisoka.

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *