Posted By Posted On

ALGERIA KUMENYANA NA NIGERIA KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI AUSTRIA

MABINGWA wa Afrika, Algeria watamenyana na Nigeria katika mchezo wa kirafiki Oktoba 9 Uwanja wa Jacques Lemans Arena mjini Sankt Veit an der Glan, Austria. 

Mechi hiyo itakuwa marudio ya Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Misri, ambayo Algeria ilishinda 2-1 Jijini Cairo.

Mchezo huo wa kirafiki utatumika kama sehemu ya maandalizi ya mechi za Novemba za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Cameroon mwaka 2021.


Kikosi cha Djamel Belmadi kitakuwa na mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Mexico siku nne baadaye nchini Uholanzi. 

Algeria kama wapinzani wao kutoka Afrika Magharibi, Nigeria walioshika nafasi ya tatu kwenye AFCON ya Misri 2019, watarejea kusaka tiketi ya fainali za Afrika mwakani zilizosimama kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.

Algeria itamenyana na Zimbabwe mwezi Novemba nyumbani na ugenini, wakati Nigeria itamenyana na Sierra Leone kama hivyo.

Les Fennecs inaongoza Kundi H kwenye mbio hizo baada ya ushindi mfululzo kwenye mechi mbili za kwanza. Algeria iliifunga Zambia 5-0 mjini Blida kabla ya kuichapa 1-0 Botswana Jijini Gaborone.

Nigeria pia inaongoza Kundi L kwa ushindi wa asilimia 100 baada ya Super Eagles kuwafunga Benin 2-1 mjini Uyo kabla ya kuifunga Lesotho 4-2 mjini Maseru.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *