Posted By Posted On

HUYU MUGALU ATAWALAZA WATU NA VIATU TU!

NA ONESMO KAPINGA

HAKIKA sijapata utamu wa mshambuliaji mpya wa Simba, raia wa DR Congo, Chris Mugalu,kutokana na jinsi anavyochezesha katika kikosi hicho.

Mugalu ni miongoni mwa wachezaji wapya wa kigeni waliosajiliwa na Klabu ya Simba katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wachezaji wengine wapya wa Simba ni pamoja na Bernard Morrison (Yanga),Larry Bwalya (Power Dynamos ya Zambia), Joash Onyango (Gor Mahia ya Kenya) na Mugalu (Lusaka Dynamos ya Zambia).

Kati ya wachezaji hao ni Mugalu ambaye hajaweza kucheza dakika 90, tangu atambulishwe na klabu hiyo ya Simba katika mchezo maalumu wa kirafiki wa Simba Day dhidi ya Vital’o ya nchini Burundi  uliochezwa Agosti 22, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Mkapa,jijini Dar es Salaam.

Simba walishinda mabao 6-0 dhidi ya wageni wao na Mugalu aliingia katika kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao moja kwenye ushindi huo.

Pamoja na kufunga bao hilo,lakini sikuona utamu wa Mugalu, kutokana na dakika chake alizopewa kucheza katika mchezo huo.

Nilitamani kuona uwezo wake zaidi katika mchezo uliofuata wa Ngao ya Jamii dhidi ya timu ya Namungo uliochezwa Agosti 31, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, lakini hakuwamo kwenye kikosi cha Simba.

Kwa muda wote, Kocha wa Simba,Sven Vandenbroeck, amekuwa akimtumia kwa dakika zote 90, Onyango huku Bwalya, Morrison na Mugalu wakati mwingine wakianzia benchi katika michezo ambayo imecheza timu hiyo.

Hata hivyo, kati ya wachezaji hao, Mugalu ndiye aliyecheza dakika chache, kwani mchezo wake wa kwanza kucheza wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulikuwa dhidi ya Biashara United, uliochezwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, mshambuliaji huyo, alitokea benchi na kufunga katika ushindi wa mabao 4-0 waliopata Simba.

Mchezo wa juzi wa Simba na Gwambina uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Mugalu alitokea benchi na kufunga bao katika ushindi wa mabao 3-0.

Kutokana na Mugalu kupewa dakika chache za kucheza tena akitokea benchi na baadaye kufunga, bado sijaona vitu adimu alivyokuwa nayo, baada ya kushindwa kucheza kwa dakika 90.

Nashindwa kusema ni mchezaji mzuri kiasi gani, kwa sababu sijamuangalia akicheza kwa dakika zote, jambo ambalo haliwezi kunipa uwezo wa kumwelezea kiwango chake.

Kwa mchezaji kama Morrison,Onyango na Bwalya naamini hakuna mwenye swali kuhusiana na viwango vyao, walivyoonesha ndani ya kikosi cha Msimbazi.

Kwa kuwa Mugalu amecheza chini ya dakika 30, natamani kumwongezea angalau acheze dakika 75 ili baadaye niweze kumwelezea alichokuwa nacho mguuni.

Inawezekana Mugalu ana vitu vingi mguuni kwake, lakini anashindwa kuonesha kutokana na kupewa dakika chache za kucheza katika kikosi chake.

Sijajua kwanini kocha wa Simba Sven anampa dakika chake Mugalu kucheza, wakati anaonekana ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga kwa staili yoyote.

Ninachoona mbele ni kwamba, Mugalu atakuja kuwalaza watu na viatu, Oktoba 18, mwaka huu, kwa kuwa akili ya wapinzani wao Yanga ipo kwa Clatous Chama, Middie Kagere, Luis Miquissone na wengineo.

Tukutane Jumatatu ijayo.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *