Posted By Posted On

MASHABIKI SIMBA WAPEWA MTIHANI

NA ZAINAB IDDY

MASHABIKI wa Simba wapo katika mtihani wa aina yake kutokana na yanayoendelea ndani ya klabu yao, yakiwa yamechochewa kwa kiasi kikubwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Wekundu wa Msimbazi hao, Barbara Gonzalez.

Mara baada ya Barbara kuteuliwa kuwa CEO wa Simba, akichukua nafasi ya Senzo Mbatha aliyejiuzulu, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kiutendaji kuanzia ndani hadi nje ya uwanja.

Kwa upande wa ndani ya uwanja, kikosi cha Simba kimekuwa kikitandaza kandanda la aina yake na kupata ushindi mnono unaoenda sambamba na burudani ya hali ya juu kutokwa kwa wachezaji wao.

Katika mechi zao mbili zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba walivuna ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Biashara United kabla ya juzi kuichapa Gwambina mabao 3-0, kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Ukiachana na ushindi huo, mashabiki wa Simba wamekuwa wakipata burudani ya aina yake kutokana na kile kinachofanywa na wachezaji wao uwanjani, kila mmoja akionyesha ufundi wa aina yake.

Kwa upande wa kiutendaji, ndani ya siku chache zilizopita, kuna mambo makubwa yamefanyika ndani ya Simba, zaidi ikiwa ni uongozi wa klabu hiyo kufanya ziara nchini Misri.

Katika ziara hiyo, Barbara aliyeongozana na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mulamu Ng’hambi, walitembelea klabu za Al Ahly na Zamalek na kubadilishana mawazo na viongozi wenzao wa vigogo hao wa soka Afrika.

Hiyo ilikuwa ni hatua kubwa na muhimu mno kwa Simba katika mkakati wao wa kujiendesha kisasa zaidi na hatimaye kuifanya klabu yao kufikia mafanikio ya wababe wa soka Afrika kama Al Ahly, Zamalek, TP Mazembe na nyinginezo.

Na katika kupigilia msumari yale yanayoendelea kufanywa na viongozi wake, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amekuja na mkakati unaolenga kuwapa raha zaidi wapenzi wa klabu hiyo.

Mkakati huo ni wazi utazidi kuwapa mzuka wapenzi wa Simba na kujikuta wakiwa katika mtihani wa kuumiza vichwa vyao kusaka fedha za kuwawezesha kupata viingilio vya uwanjani kuishuhudia timu yao ikicheza na kusamehe mahitaji mengine kama chakula na kadha wa kadha.

Kwa mujibu wa kocha huyo, kwa mikakati aliyoipanga, hakuna shabiki wa Simba atakayekuwa tayari kukosa uwanjani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Sven alisema kuwa amekuja na mkakati mpya utakaomwezesha kila mchezaji wake kufunga bao, lengo likiwa kupata idadi kubwa ya mabao na kuwapa raha mashabiki wao.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kutimiza kile tulichokubaliana baada ya kuanza kucheza mechi za nyumbani, hii ni fahari kwa Simba kuona tuna wachezaji waelewa na wenye kutimiza majukumu yao.

“Idadi hii ya mabao katika mechi moja, itakuwa endelevu hata katika michezo yetu ya ugenini, katika hilo, kila mchezaji atakayepata nafasi ya kufunga ni lazima afanye, bila ya kuangalia anacheza nafasi gani.

“Sitaki kutegemea mabao kupitia washambuliaji pekee; iwe beki, kiungo hata kipa, akipata nafasi ya kufunga, nataka afunge. Tunahitaji mabao mengi msimu huu  ambayo yatakuja kuwa na faida kwetu hapo baadaye na kuwapa mashabiki kile wanachokitarajia kutoka kwetu,” alisema Sven.

Akizungumzia mchezo wao wa juzi, Sven alisema: “Ulikuwa mgumu tofauti na ule tuliocheza na Biashara, Gwambina walijipanga kuja kutudhibiti, nawapongeza kwa hilo, lakini bado hawakuweza kutuzuia kufanya kile tulichohitaji.

“Wachezaji watapumzika kwa siku moja ya Jumapili (jana) na Jumatatu (leo), tutaendelea na mazoezi kujiandaa na mechi inayokuja dhidi ya JKT Tanzania, tukienda kucheza ugenini.”

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *