Posted By Posted On

UONGOZI YANGA WAKEMEA MASHABIKI, VITENDO VISIVYO VYA KIUNGWANA

Msomaji wa Yanganews Blog:Uongizi wa Klabu ya Yanga umevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza kwa kina ili kuwabaini mashabiki wao waliowafanyia fujo mashabiki wa Simba, katika mchezo wa jana Septemba 27, 2020 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Jana mara baada ya mchezo wa Yanga na Mtibwa Sugar uliopigwa kwenye imba la Jamhuri mjini Morogoro na Yanga kushinda kwa bao 1-0, mashabiki wa klabu hiyo walifanya vurugu huku video zilizoonyesha tafrani hiyo zikisambaa katika mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Yanga asubuhi hii, umelaani na kukemea kitendo hicho huku ukivitaka vyombo vya sheria kuwachukulia hatua endapo itawabaini waliofanya vitendo hivyo.

“Uongozi umesikitishwa na kitendo kisicho cha kiungwana kilichofanywa na baadhi ya mashabiki cha kuwapiga na kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba waliofika Uwanja wa Jamhuri jana,” ilisema taarifa ya klabu hiyo.

”Pamoja na kusikitishwa pia uongozi unalaani vikali tabia hiyo inayojengeka ya uvunjifu wa amani katika soka, na kuviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza na hatimaye kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.”

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa Yanga inaamini mpira sio uadui bali ni furaha na  hivyo inawakumbusha mashabiki kuwa upinzani wao na Simba unatokana na utani wa jadi na sio uhasama.

Mbali na hayo, uongozi uliwashukuru pia mashabiki waliojitokeza katika mchezo huo na kufanikiwa kupata ushindi.

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *