Posted By Posted On

Wachezaji Simba wapewa nondo za Al Ahly

ASHA MUSSA NA GODFREY PAUL (TUDARCo)

WACHEZAJI wa Simba wamepewa semina bab kubwa inayolenga kuwajenga zaidi ili kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Semina hiyo iliwahusu pia wafanyakazi wengine wa klabu hiyo, likiwamo benchi la ufundi, ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez.

Wataalam mbalimbali, walizungumza katika semina hiyo iliyofanyika kwenye kambi ya wachezaji iliyopo jijini Dar es Salaam, huku Barbara akishuka nondo alizozipata wakati wa ziara yake nchini Misri, alikotembelea klabu za Al Ahly na Zamalek za huko.

Mbali ya Barbara, wengine ‘walioshusha madini’ katika semina hiyo ni Mkuu wa Idara ya Uendeshaji Simba, Dk. Arnold Kashembe na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi.

Mwingine aliyewapa darasa wachezaji na wafanyakazi wa Simba katika semina hiyo ni mjasiriamali, Anthony Luvanda aliyezungumzia juu ya matumizi ya fedha na namna ya kuweka akiba.

Pamoja na semina hiyo, wachezaji na wafanyakazi wa Simba walipata nafasi ya kushiriki michezo mbalimbali iliyokuwa na lengo ya kuboresha uhusiano wa kikazi.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *