Posted By Posted On

Adui wa Kagere atajwa

NA ZAINAB IDDY

KINARA wa mabao wa Ligi kuu Tanzania Bara wa muda wote, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, amemtaja adui wa Meddie Kagere wa Simba katika vita ya kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu.

Akizungumza na BINGWA jana, Mmachinga anayeshikilia rekodi ya ufungaji mabao Ligi Kuu Bara kwa kucheka na nyavu mara 26, alisema kuwa Prince Dude wa Azam FC  utaleta upinzani wa hali ya juu kwa Kagere.

Dube tangu asajiliwe na Azam msimu huu, amekuwa na kiwango kizuri, akifunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao katika michezo minne aliyoichezea timu hiyo.

Katika michezo hiyo minne aliyoichezea, alifunga mabao mawili dhidi ya Coastal Union kabla ya kutikisa nyavu za Tanzania Prisons.

Baada ya kuona ubora wake katika kucheka na nyavu, Mmachinga alisema kuwa Dude ni usajili bora kwa Azam, lakini pia atatoa changamoto kwa washambuliaji wengine wenye malengo ya kuwa wafungaji bora mwisho wa msimu.

“Dude ni usajili bora kwa Azam ukizingatia ni mzoefu wa mashindano ya kimataifa, katika mechi tatu alizocheza, ameonyesha ana macho ya kuliona lango la wapinzani.

“Binafsi namtabiria kuwa mfungaji bora msimu huu, bila shaka msimu huu Kagere amepata mpinzani wake katika harakati zake za kuwa mfungaji bora kwani tayari ameonyesha kuwa na uchu wa kuchukua kiatu cha dhahabu kwa msimu mwingine,” alisema Mmachinga.

Mbali ya Dude, wafungaji wengine wa Ligi Kuu Bara wenye mabao zaidi ya moja ni Kagere akiwa na mawili kama ilivyo kwa Chris Mugalu na Mzamiru Yassin (Simba), Marcel Kaheza (Polisi Tanzania), Reliats Lusajo na Hassan Kabunda (KMC) pamoja na Lamine Moro  wa Yanga.

Tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara kwa sasa inashikiliwa na Kagere ambaye msimu wa 2019/20 alitupia jumla ya mabao 22, kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *