Posted By Posted On

BALAMA AZUNGUMZIA MAJERUHI YAKE YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Wakati maandalizi ya mechi ya kwanza ya Kariakoo msimu huu yakianza kupamba moto, Kipenseli amezungumza na chanzo chetu kuhusu maisha yake ya soka.

Kiungo huyu ambaye kwa sasa ni majeruhi, ameweka wazi sababu za yeye kuitwa kipenseli kuwa ni kutokana na ufupi.

“Hili jina nimepewa na wachezaji wenzangu wa zamani wa Alliance tulipokuwa tunacheza pamoja na kusoma pamoja, waliamua kuniita hivyo kwa madai kuwa mimi ni mfupi kama penseli, ndio limekua hadi sasa siwezi kukataa kwani ni kweli mimi ni mfupi,” anasema.

Sio kila mzazi anatamani kugundua kipaji cha mwanaye mapema kama ilivyo kwa nchi za wenzetu. Kwa upande wa Watanzania wengi wamekuwa wakiamini katika elimu na kujikuta wakiua vipaji wa watoto wao.

“Haikuwa kazi rahisi kucheza soka kwani baba alikuwa hataki kusikia najihusisha nalo, ni mama pekee ambaye alikuwa anaunga juhudi zangu kwenye mpira,” anasema Mapinduzi na kuongeza:

“Kuna muda nilikuwa natoroka nyumbani kwenda kucheza mpira, lakini kitu kikubwa nilichokuwa nahofia ni kuumia nikiwa uwanjani kwani nilikuwa naogopa nitarudi vipi na nani ataniuguza jambo ambalo lilikuwa linanifanya nicheze kwa nidhamu zaidi.”

Anasema nidhamu hiyo imemsaidia hadi leo katika soka la juu ambapo kufikia sasa ameonyeshwa kadi nyekundu mara moja tu tena akiwa na Yanga kwenye mchezo dhidi ya Pyramids alipobishana na mwamuzi baada ya mchezo.

“Nikiwa Alliance nimecheza mechi zote dakika 90, na sikuwahi kuonyeshwa hata kadi ya njano,” anasema.

“Hata Yanga nimeendeleza nidhamu yangu, nimecheza ligi bila kupata hata kadi ya njano, nafurahia mpira ndio ajira yangu, naahidi kuendeleza ili kumridhisha baba yangu na mashabiki zangu.”

Akizungumzia Yanga ya msimu huu, Balama anasema wana kikosi bora.

“Ni moja ya usajili bora kuwahi kutokea Yanga, wamesajili kutokana na upungufu uliokuwapo, nimefurahishwa na uwezo wa nyota wengi wapya, mashabiki wategemee mambo mazuri waendelee kutupa ushirikiano,” anasema.

“Sina wasiwasi na kipaji changu, sibahatishi, ni mpambanaji, bado naiona nafasi yangu kwenye kikosi cha kwanza, kikubwa natakiwa kuongeza juhudi mazoezini ili niweze kurudi kwenye majukumu yangu ya kawaida na nina imani hilo linawezekana.”

Kiungo huo alivunjika mfupa mdogo wa goti akiwa mazoezini baada ya kuangukia mpira akiwa katika harakati za kutaka kuupiga.

“Sikusukumwa na mtu, ni katika harakati zangu za kutaka kupiga mpira niliteleza na kuuangukia kwa mguu tukio ambalo lilinishtua na kuambiwa nimevunjika, haikuwa rahisi kuamini hapohapo hadi maumivu yaliponizidi,” anasema na kuongeza:

“Nilivunjika mfupa mdogo wa mguu wangu wa kushoto na sasa naendelea vizuri, naushukuru uongozi wangu kwa juhudi walizozifanya kuhakikisha natibiwa kwa uangalizi wa hali ya juu, sasa naendelea vizuri.”

Wakati ukijiuliza jeuri ya Balama katika soka iko wapi hadi anasema nafasi yake kikosini ipo palepale? Lakini pamoja na moto ulionekana kutoka kwa nyota wapya kumbe jamaa anaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani.

“Kweli naweza kukosa namba kwenye nafasi zote ninazoweza kucheza namba mbili, saba, kumi na kumi na moja lazima nitapata nafasi tu kwa sababu mpira nauweza.” anasema

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *