Posted By Posted On

PASI YA MORRISON YAFUMUA KIKOSI

NA ZAINAB IDDY

PASI aliyopiga Bernard Morrison wa Simba na kuzaa bao lililofungwa na Chris Mugalu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Gwambina, imefumua kikosi cha timu hiyo inayonolewa na Sven Vandenbroeck.

Mchezo huo ulichezwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na Simba kushinda mabao 3-0.

Morrison aliyeingia uwanjani dakika ya 67, akichukua nafasi ya Larry Bwalya, akiwa nje kidogo ya eneo la 18 kushoto mwa dimba hilo, alipiga pasi maridadi iliyomkuta Mugalu na mshambuliaji huyo raia wa DR Congo kucheka na nyavu.

Kama ilivyokuwa kwa Morrison, Mugalu naye alitokea benchi kuchukua nafasi ya Meddie Kagere dakika ya 75.

Mabao mengine ya Simba katika mchezo wao huo wa nne wa Ligi Kuu Bara, yalifungwa na Kagere dakika ya 39 akimalizia pasi ya Luis Miquissone, huku lingine likiwekwa kimiani na beki Serge Pascal Wawa dakika ya 50 kwa mpira wa adhabu baada ya Bwalya kufanyiwa madhambi umbali wa takribani mita 30.

Ushindi huo, uliwawezesha mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo kufikisha pointi 10 na kushika nafasi ya pili nyuma ya vinara Azam FC wenye pointi 12.

Kutokana na kiwango kinachoendelea kuonyeshwa na Morrison, benchi la ufundi la Simba na hata viongozi wa klabu hiyo, wameonekana kukunwa mno na Mghana huyo waliyemtwaa kininja kutoka Yanga.

Akizungumza na BINGWA jana, Sven alisema kuwa kiwango cha Morrison kimebadili mwelekeo wa kikosi chake tofauti na ilivyokuwa kabla ya ujio wa mkali huyo ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao.

Sven alisema kuwa anaamini siri kubwa ya mafanikio ya Morrison na kikosi chake kwa ujumla ni upendo miongoni mwa wachezaji wake na Wanasimba kwa ujumla.

“Timu inapata ushindi wa mabao mengi si kwa sababu ya mafundisho ninayotoa, bali ni umoja na kutokuwepo kwa ubinafsi kwa wachezaji wanapokuwa uwanjani.

“Ndani ya timu, upendo na mshikamano umeongezeka kwa hali ya juu na kuthibitisha hilo, angalia bao alililofunga Chris  Mugalu katika mchezo na Gwambina, ni wazi Bernard Morrison alikuwa kwenye nafasi sahihi ya kufunga, lakini aliamua kutoa pasi ya mwisho kwa mwenzake, huu ni upendo na ushirikiano mkubwa.

“Wachezaji wote wanafanya vizuri na nina furaha katika hilo, kwa sasa sina wasiwasi tena, ni suala la kuamua tu, leo unamchezesha huyu, kesho yule na bado unakuwa na uhakika wa ushindi, tena mnono.

“Lakini itakuwa vizuri tukiwa katika kiwango kikubwa zaidi kwenye mechi inayofuata kuhakikisha tunatoka na ushindi, tena wa idadi kubwa ya mabao zaidi ya michezo iliyotangulia,” alisema.

Kocha huyo aliongeza: “Kwa soka la kisasa, hata kama utafanya usajili wa kuwaleta wachezaji kutoka sehemu ambayo kuna kiwango kikubwa cha soka, lakini kukiwa na wachezaji wabinafsi wanaohitaji kuonekana wao bora zaidi ya wengine, hutaweza kupata ushindi ambao kwa sasa Simba tunaupata. 

“Kuanzia mechi inayokuja, timu yangu itakuwa inaingia na mbinu mpya mara kwa mara, lengo ni kutotoa nafasi kwa wapinzani wetu kutukariri, lakini pia kuna nguvu tutakayoiongeza ambayo itakuja kutusaidia kupata kile tunachokihitaji mbele ya JKT Tanzania.”

Simba jana ilianza mazoezi ya ‘gym’ kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Bara unaofuata dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *