Posted By Posted On

CHILUNDA WA AZAM FC APATA BAHATI NYINGINE, KUJIUNGA NA MOULOUDIA OUJDA YA MOROCCO

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Iddi Chilunda anatarajiwa kusaini mkataba wa kujiunga na Mouloudia Oujda ya Ligi Kuu ya Morocco.
Azam FC leo imesema kwamba imefikia makubaliano ya kumuacha mchezaji wake huyo aende Mouloudia D’oujda kukamilisha taratibu za mwisho za kujiunga na miamba hiyo ya soka Morocco.
Akijiunga na klabu hiyo, Chilunda atakuwa mchezaji wa tatu wa Kitanzania katika ligi ya Morocco baada ya beki wa kushoto, Nickson Kibabage na viungo Simon Msuva wote wanachezea Difaa Hassan El Jadida na Maka Edward wa Moghreb Tetouan.

Shaaban Iddi Chilunda anatarajiwa kujiunga na Mouloudia Oujda ya Ligi Kuu ya Morocco

Msuva mwenye umri wa miaka 26 sasa, ndiye aliyefungua mlango wa Watanzania katika Ligi ya Morocco baada ya kujiunga na Difaa El Jadida mwaka 2017 akitokea Yanga ya Dar es Salaam, akafuatiwa na Kibabage kutoka Mtibwa Sugar mwaka jana na Maka aliyetokea Yanga pia mwaka jana.
Chilunda aliibukia katika tmu ya vijana ya Azam FC mwaka 2012 kabla ya kucheza mechi yake ya kwanza timu ya wakubwa mwaka 2016 na Agosti 7 mwaka 2018 akajiunga na CD Tenerife ya Hispania katika Segunda División (Daraja la Kwanza) kwa mkataba wa miaka miwili.
Lakini mambo hayakumuendea vizuri huko, akatolewa kwa mkopo kwenda  CD Izarra ya Segunda División B (Daraja la Tatu) kabla ya kurejea Azam FC mwaka huu.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *