Posted By Posted On

Mamilioni yamwagwaYanga kisa Morrison

NA ZAINAB IDDY

MAMBO ni bam bam Yanga kwani leo mamilioni ya fedha yanatarajiwa kumwagwa ndani ya kikosi cha Wanajangwani hao, huku Bernard Morrison akichangia hilo.

Mamilioni hayo wapewa wachezaji, ikiwa ni siku moja baada ya kupata ushindi mnono wa kwanza wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa tano wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam juzi.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kufikisha pointi 13 kutokana na mechi tano, ikilingana pointi na watani wao wa jadi, Simba, waliopo juu yao kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.

Mchezo unaofuata wa Yanga katika ligi hiyo, utakuwa ni dhidi ya Simba utakaochezwa Oktoba 18, mwaka huu Uwanja wa Mkapa.

Kwa kufahamu ugumu na umuhimu wa mchezo huo, huku wakiwa na hasira na nyota wao wa zamani, Morrison aliyetimkia Msimbazi, mabosi wa Yanga wameamua kufanya kweli kwa kumwaga milioni 20 katika kikosi chao.

Habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zilizonaswa na BINGWA jana, zinasema kuwa wadhamini wa klabu hiyo, GSM, walitenga kitita cha shilingi milioni 50 kwa benchi la ufundi na wachezaji, wakipanga kuzitoa iwapo timu hiyo itaichapa Simba.

Lakini pia, mabosi wa klabu hiyo waliahidi kuwapa wachezaji wao shilingi milioni 20 iwapo wangeshinda mechi nne mfululizo za ligi kabla ya kuwavaa watani wao hao wa jadi.

“Kesho (leo) ahadi ya kwanza ya shilingi milioni 20, inatimizwa, hii ni ile iliyotolewa iwapo tungeshinda mechi nne mfululizo ambazo tumeshinda. Baada ya hapo, kuna mambo mazuri zaidi yanakuja kuelekea mchezo wetu na Simba,” alisema mmoja wa vigogo wa Yanga akiliambia BINGWA jana.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga upo katika mkakati wa kuwaongezea wachezaji wake saba mikataba mipya, akiwamo kiungo Haruna Niyonzima.

Niyonzima alijiunga na Yanga msimu uliopita kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu utakaofika ukingoni mwishoni mwa msimu huu.

Wachezaji wengine waliopata zali hilo ni ni Deus Kaseke, Metacha Mnata, Farouk Shikalo, Abdullaziz Makame, Juma Makapu na Mapinduzi Balama.

Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa suala hilo la usajili linatarajiwa kufanyika mara baada ya kumalizika kwa mechi yao na Simba, Oktoba 18, mwaka huu.

“Mikataba ya wachezaji hao tayari ipo mikononi mwa Hersi Said (Mkurugenzi wa GSM na Makamu Mwenyekiti wa Usajili Yanga) na tumeamua kufanya hivyo ili kupunguza presha pale ile ya awali itakapomalizika mwisho wa msimu.

“Tumeona kile kilichotokea kwa Bernard Morrison aliyesajiliwa na Simba, hatuhitaji tena mambo kama haya yajitokeze, mara baada ya mechi yetu na watani kumalizika, tutawaita wachezaji mmoja mmoja kuangalia namna gani tutaboresha mikataba yao mipya,” alisema bosi huyo aliyepo katika Kamati ya Mashindano ya Yanga.

Hivi karibuni mara baada ya Yanga kumwongeza mkataba mpya wa miaka miwili na nahodha wao, Lamine Moro, Hersi alinukuliwa akisema kuwa mchakato wa kufanya hivyo kwa wachezaji wao ni endelevu, hususan wale waliopo katika viwango bora.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *