Posted By Posted On

Mukoko amtumia ujumbe Chama

NA ZAINAB IDDY

KIUNGO wa Yanga, Mukoko Tonombe, amesema kuwa anaisubiri kwa hamu mchezo wao dhidi ya Simba, akipania kupimana ubavu na nyota wa watani wao hao wa jadi, akiwamo Clatous Chama.

Simba na Yanga, zitashuka dimbani kuumana katika mchezo wa Ligi Kuu  Tanzania Bara, utakaochezwa Oktoba 18, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. 

Mukoko amejiunga na Yanga msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Tangu atue Jangwani, Mukoko anayecheza nafasi ya kiungo, amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi hicho, huku akifanikiwa kukifungia bao moja katika michezo minne ya Ligi Kuu Bara aliyovaa jezi ya kijani na njano.
Mukoko ameliambia BINGWA kuwa anaitamani siku hiyo kutokana na simulizi nyingi anazozisikia kuhusu mechi ya Simba na Yanga.

“Wachezaji wenzangu wananisimulia mambo mengi kuhusu mechi ya Simba na Yanga, kinachonivutia zaidi ninavyosimuliwa kuhusu mashabiki.

“Naamini itakuwa mechi nzuri na ya kawaida wala sio ngumu kama wanavyoizungumzia, kwa mara ya kwanza nitakapocheza mchezo huo nataka kuwaonyesha jinsi gani mpira unachezwa na vipi unaweza kuuona mchezo wa ‘derby’ (wapinzani) ni wa kawaida tofauti na wenzangu wanavyouchukulia,” alisema Mukoko.

Mbali ya Chama, viungo wengine wa Simba watakaopambana na Mukoko ni Luis Miquissone, Larry Bwalya, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, Muzamiru Yassin na wengineo.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *