Posted By Posted On

SIMBA HII UTATOKAJE

NA ASHA KIGUNDULA- DODOMA

KWA Simba hii, kazi ipo msimu huu kwani walichoifanyia JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma jana, wapinzani wao wajao, wakiwamo Yanga, wajipange hasa.

Mbao mawili ndani ya dakika tano, si kitu cha mchezo mchezo. Ndivyo ilivyokuwa kwa Simba jana kwani dakika tatu tu tangu mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara umeanza, waliandika bao lao la kwanza lililofungwa na Meddie Kagere.

Dakika mbili baadaye, mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo, waliongeza bao lingine kupitia kwa Chris Mugalu kabla ya Kagere na Luis Miquissone kucheka nyavu kuiwezesha Simba kuvuna ushindi wa mnono wa mabao 4-0 dhidi ya wenyeji wao hao.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 13, sawa na Yanga, ikiwa ni baada ya timu zote hizo kucheza mechi tano.

Azam ambayo jana usiku iliifunga Kagera Sugar mabao 4-2 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ipo kileleni mwa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 15.

Kwa upande wao, JKT Tanzania kwa kupoteza mchezo wa jana, imebaki na pointi nne baada ya kucheza mechi tano.

Simba iliuanza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kuandika bao la kwanza la mpira wa kichwa kupitia kwa Kagere kutokana na pasi murua kutoka kwa kiungo Larry Bwalya.

Bao hilo liliwaongezea morali wachezaji wa Simba na hatimaye kuongeza lingine dakika ya tano kupitia kwa Mugalu aliyefunga kwa kichwa kutokana na krosi ya Luis.

Baada ya bao hilo la pili la Simba, JKT Tanzania walizinduka na kuwabana wageni woa hao kuepuka kuongezwa mabao mengine zaidi, lakini pia wakisaka ya kusawazisha.

Katika jidihada hizo. Mchezaji wa JKT Tanzania, Richard Maranya, alionyeshwa kwa kadi ya njano dakika ya 35, baada ya kumfanyia madhambi kiungo wa Simba, Jonas Mkude.

Mchezo huo ulioendelea kuwa mkali na wa kusisimua, huku viungo wa Simba, Clatous Chama, Luis na Bwalya, wakigongeana vema, huku Kagere na Mugalu wakizidi kuwatia hofu mabeki wa JKT Tanzania.

Dakika ya 40, Kagere aliifungia Simba bao la tatu kwa shuti kali la mguu wa kushoto, ikiwa ni  baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Bwalya, Clatous Chama na Luis.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa Simba kuwa mbele kwa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Kwa ujumla kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi, Hance Mabena kutoka Tanga, Simba ilitawala na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa JKT Tanzania.

Kipindi cha pili, Simba iliingia uwanjani na mpango kazi ule ule wa kushambulia kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la nne dakika ya 53, lililowekwa kimiani na Luis kwa mkwaju wa mbali.

Dakika ya 50, kipa wa JKT Tanzania, Patrick Muntari alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Luis aliyeisumbua mno safu ya ulinzi ya wenyeji wao hao.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, alifanya mabadiliko dakika ya 59 kwa kumtoa Kagere aliyeumia na kumwingiza kiungo Muzamiru Yassin.

Dakika ya 72, beki wa kati wa Simba, Pascal Wawa, alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Mohamed Nurdin wa JKT Tanzania.

JKT ilifanya mabadiliko dakika ya 58, akitoka Maranya na nafasi yake  kuchukuliwa na Danny Lyanga kabla ya dakika ya 61 Mugandila Shaban wa timu hiyo kumpisha Kelvin Nashon.

Dakika ya 73, Sven alimtoa Chama na nafasi yake kuchukuliwa na Bernard Morrison kabla ya Luis kumpisha Hassan Dilunga.

Kwa kifupi, mfumo wa Simba wa kutumia washambuliaji wawili, Kagere na Mugalu, ndio ulioibeba timu hiyo jana kwani mabao mawili ya haraka waliyofunga, yalionekana kuwavuruga mno JKT Tanzania.

Inadaiwa kuwa mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, amekuwa akitamani kocha wao kupanga washambuliaji wawili kwa pamoja badala ya mmoja kama ilivyokuwa katika mechi zao zilizopita.

Katika mchezo mwingine uliochezwa jana jioni, Biashara United, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Raundi ya tano ya ligi hiyo, itahitimishwa leo kwa mchezo mmoja kati ya KMC na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. 

Kikosi cha JKT Tanzania: Patrick Muntary, Michael Aidan, Nurdin Mohamed, Frank  Nchimbi, Edson Katanga, Richard Maranya/Daniel Lyanga (dk58), Mgandila Shaaban/Kelvin Nashon (dk61), Daniel Mecha, Kelvin Sabato, Adam Adam na Mwinyi Kazimoto.

Simba SC: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussien ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone/Hassan Dilunga (dk77), Larry Bwalya, Meddie Kagere/Muzamil Yassin (dk59), Chriss Mugalu na Clatous Chama/Bernard Morrison (dk73).

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *