Posted By Posted On

CARLINHOS APEWA ONYANGO

NA MOHAMED KASSARA

MIKAKATI ya kuelekea Oktoba 18, mwaka huu, imeanza kusukwa Yanga tayari kuwakabili watani wao wa jadi, Simba katika mchezo wa raundi ya sita wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Moja ya eneo ambalo Yanga wameanza kushughulika nayo ni safu ya ulinzi ya Simba na kazi hiyo amekabidhiwa kiungo fundi, Cralos Carlinhos ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Wanajagwani hao kwa sasa.

Idara ya ufundi ya Yanga inayoundwa na makocha, wachezaji wa zamani na watalaamu wa soka nchini, imechunguza kwa makini safu hiyo ya ulinzi inayoongozwa  na Pascal Wawa na Joash Onyango, wakabaini Carlinhos ndiyo atawatosha.

Wawa na Onyango wamecheza pamoja kama mabeki wa kati katika michezo mitatu mfululizo bila kuruhusu wavu wao kutikishwa.

Wakali hao walianza kucheza sambamba katika mchezo dhidi ya Biashara United, ambao Simba  ilivuna ushindi wa mabao 4-0, wakacheza dhidi ya Gwambina katika ushindi wa mabao 3-0, kabla ya kuanza pamoja tena juzi dhidi ya JKT Tanzania na timu hiyo kushinda mabao 4-0.

Hata hivyo, jopo hilo la ufundi limeaza kumwelekeza Carlinhos jambo la kumfanyia Onyango ambaye ndiye anaonekana muhimu mpya wa idara hiyo kutokana na kuanza katika michezo yote mitano.

Carlinhos ambaye ni mtalaamu wa kuchezea mpira na kupiga mipira ya hatari kwenye lango la wapinzani, amepewa jukumu la kuhakikisha anamtoa mchezoni Onyango ili kuwarahisishia kazi Michael Sarpong na Yacouba Sogne kumtungua kipa Aishi Manula.

Muangola huyo ambaye ametengezea mabao mawili ya Yanga na kufunga bao moja katika michezo mitatu iliyopita, anapewa maagizo maalumu ya kumfanya Wawa au Onyango apaniki ili apewe kadi au kutolewa kanisa nje ya uwanja.

Wakati Carlinhos akiwa na kazi hiyo, winga matata, Tuisila Kisinda atakuwa na jambo lake na beki wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ katika upande wa kushoto.

Kisinda ambaye anasifika kwa uwezo mkubwa wa kulamba chenga mabeki, amepania kumshikisha adabu Tshabalala anayecheza upande wa beki wa kushoto.

Mcongoman huyo tayari ameshafanyia hivyo mabeki wengine kama David Luhende wa Kagera Sugar na Hassan Kessy wa Mtibwa.

Kisinda amepanga ‘kumlambisha mchanga’ Tshabalala, huku pia akiwa tayari kumwonyesha kazi Wawa iwapo atajipendekeza kumkaba.

Naye, Mukoko Tonombe, yeye atakuwa katikati ya dimba kuchuana na viungo wa Simba, Clatous Chama na Luis Miquissone, lakini pia Bernard Morrison.

Tayari Mukoko amekiri kuwatamani akina Chama, akitamba siku hiyo patachimbika.

“Nimekuwa nikisimuliwa juu ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga, natamani Oktoba 18 ifike haraka niwape raha mashabiki wa timu yangu. Najua Simba ina viungo wazuri, ila mbele yangu hawatafurukuta,” alisema.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *