Posted By Posted On

UKIZUBAA UNAPIGWA Hivi hapa vipigo vikali zaidi EPL karne ya 21

MANCHESTER, England

LIGI Kuu England inatambulika kama moja ya ligi ngumu na yenye ushindani mkubwa duniani ambayo imezungukwa na timu nyingi zenye uwezo na wachezaji bora.

Ni kweli, lakini mara kadhaa imekuwa ikishangaza kutokana na matokeo ya kikatili na udhalilishaji ambayo yamekuwa yakipatikana ndani yake.

Juzi, ilikuwa siku ya kushangaza kwa vigogo wa soka la England, Manchester United na Liverpool kupata vipigo vya aibu kutoka kwa Tottenham na Aston Villa kwa kufuatana.

Manchester United iliyokuwa katika Uwanja wa Old Trafford,  ilikubali kichapo cha aibu cha mabao 6-1 kutoka kwa Tottenham huku Aston Villa wakitumia vizuri Uwanja wa Villa Park, kuichakaza Liverpool kwa mabao 7-2.

Makala hii inakuletea matokeo 10 ya kushangaza yaliyowahi kutokea katika karne ya 21 ndani ya Ligi Kuu England.

Tottenham Hotspur 9-1 Wigan Athletic (2009)

Ilibaki kidogo Tottenham waifikie rekodi ya Manchester United ambao walishinda mabao 9-0, miaka 15 kabla ya mechi hiyo, lakini walishindwa kufanya hivyo.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Tottenham walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0, lakini ilikuwa dhahama kipindi cha pili ambacho straika Jermaine Defoe alifunga mabao matano.

Kilikuwa kipigo cha aibu kwa wageni, lakini, baadae mabosi wa Wigan waligharamia tiketi za mashabiki ambao walisafiri kwenda kushuhudia mchezo huo.

Southampton 8-0 Sunderland (2014)

Sunderland walikuwa na hali mbaya kabla ya kushuka daraja mwaka 2017. Lakini, Southampton walikuwa moto wa kuotea mbali miaka mitatu nyuma kwa kuidhalilisha klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Light.

Graziano Pelle alifunga mara mbili jioni ile, huku wengine ambao ni Jack Cork, Dusan Tadic na Victor Wanyama waliifungia Southampton. Jambo la kushangaza, hayo mabao matatu mengine yalikuwa yakujifunga.

Newcastle United 5-1 Tottenham Hotspur (2016)

Bado kinaendelea kuwa kidonda kilichokatiza mbio za ubingwa wa Ligi Kuu na ikiwezekana kumaliza nafasi ya pili, juu ya Arsenal kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 10. Tottenham walitakiwa kushinda dhidi ya Newcastle United ambao walikuwa tayari wameshuka daraja ili kujiwekea nafasi nzuri.

Hata hivyo, ilikuwa siku tofauti kwa Tottenham iliyokuwa ikifundishwa na Mauricio Pochettino, ambaye alisema hiyo ilikuwa siku mbaya tangu aanze kufundisha soka, kwani walifungwa mabao 5-1 na Newcastle iliyokuwa pungufu uwanjani.

Middlesbrough 8-1 Manchester City (2008)

Ingawa, Manchester City inaonekana kuwa timu ya hatari baada ya waarabu kuinunua, lakini hili haliwezi kusahaulika. Siku ya mwisho ya msimu wa 2007/08, Middlesbrough walifanya mauaji mazito.

Richard Dunne, alionyeshwa kadi nyekundu mapema na kuacha pengo katika safu ya ulinzi, hali iliyopelekea wenyeji kulitumia kwa faida na nyota Afonso Alves alifunga mabao matatu ‘hat trick’ kabla ya Elano Blumer kufanya hivyo kwa mara ya pili ndani ya mchezo huo.

Chelsea 6-0 Arsenal (2014)

Washika Bunduki walikuwa wakipata vipigo vya kudhalilishwa kipindi cha mwisho cha Arsene Wenger, lakini hiki cha mabao 6-0, kilitokea katika mchezo wa 1000 wa kocha huyo wa Ligi Kuu.

Mchezo ulikuwa wa presha kubwa, Jose Mourinho na Wenger walikunjana mashati, Chelsea waliiharibu siku hizo na itakumbukwa Arsenal walikuwa pungufu baada ya dakika ya 15 beki wa kushoto Kieran Gibbs,  kuonyeshwa kadi nyekundu.

Manchester City 6-0 Chelsea (2019)

Chelsea ni moja ya timu bora ndani ya Ligi Kuu England, lakini mwaka jana, walikuwa na siku mbaya ndani ya Uwanja wa Etihad baada ya kuchapwa mabao 6-0 na Manchester City ambao walifungwa mabao 2-0, mchezo uliopita.

Ilikuwa hatari, ilipofika dakika ya 30, vijana wa Pep Guardiola walikuwa mbele kwa mabao 4-0, huku straika Sergio Aguero akifunga mabao matatu ‘hat trick’.

Manchester United 8-2 Arsenal (2011)

Arsenal walikuwa wakiandamwa na wachezaji wengi wenye majeraha kabla ya mchezo huo, lakini, ilibidi wasafiri kwenda Old Trafford pasipokuwa na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza. Haiwezi kuwa kisingizio.

Kirahisi tu, Arsenal walizamishwa ndani ya maji kama kikombe, Wayne Rooney alikuwa moto wa kuotea mbali kwa kufunga mabao matatu ‘hat trick’ huku Theo Walcott na Robin van Persie wakifunga mabao ya kufutia machozi kwa Washika Bunduki.

Stoke City 6-1 Liverpool (2015)

Liverpool walikuwa na mpango wa kumuaga vizuri nahodha wao Steven Gerrard, lakini Stoke City waliharibu sherehe hiyo kwa kuwanyuka Majogoo mabao 6-1,  huku kipindi cha kwanza wakiongoza kwa mabao 5-0.

Hata hivyo, Gerrard alifunga bao la kufutia machozi kwa Liverpool kabla ya straika wa zamani wa timu hiyo, Peter Crouch kupigilia msumari wa sita katika jeneza hilo.

Southampton 0-9 Leicester City (2019)

Leicester City chini ya Brendan Rodgers wamekuwa moto wa kuotea mbali, Oktoba, mwaka jana aliifikia rekodi ya Manchester United ya kushinda mabao mengi katika Ligi Kuu England. Wakali hao waliifumua Southampton kwa mabao 9-0 , huku Jamie Vardy na Ayoze Perez kila mmoja akifunga hat trick.

Southampton walizama mapema baada ya beki wao Ryan Bertrand kutolewa nje kwa kuonyeshwa kadi nyekundu mapema. Pia, huu ni ushindi mkubwa zaidi ugenini ndani ya Ligi Kuu England, lakini Saints walilipa kisasi kwa kushinda mabao 2-1, mchezo wa marudiano uliochezwa King Power.

Manchester United 1-6 Manchester City (2011)

Matokeo ya mchezo huo yalikuwa ya kuumiza Sir Alex Ferguson, akiiangalia saa yake na kugundua muda umeganda, mshale wa sekunde ulikuwa ukitembea taratibu mithiri ya kobe. Haiwezi kusahaulika.

Roberto Mancini alituma onyo kali kwa wenyeji wao ndani ya Old Trafford katika mbio za ubingwa, hicho kilikuwa kipigo kikali zaidi nyumbani kwa Manchester United tangu mwaka 1955.

Edin Dzeko na Mario Balotelli wote walifunga mara mbili, huku straika huyo raia wa Italia,  akionyesha shati aliyovaa ndani ya jezi ikiwa imeandikwa ‘Why always me?’ yaani ‘Kwanini kila wakati mimi?’

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *