Posted By Posted On

Yanga yaingia kambini kuiwinda Simba

NA ZAINAB IDDY

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuingia kambini leo kuanza maandalizi ya kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba.

Yanga itakuwa mwenyeji wa mchezo huo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Oktoba 18, mwaka huu.

Wachezaji wa timu hiyo, chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi, wanatarajiwa kukutana klabuni kwao Jangwani, Dar es Salaam leo mchana tayari kwenda katika kambi yao iliyopo Kijiji cha Maraha, Avic Town, Kigamboni.

Akizungumza na BINGWA jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga, Hassan Bumbuli, alisema wachezaji wao walipewa mapumziko ya siku mbili baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi dhidi ya Coastal Union.

“Baada ya mechi na Coastal, tulitoa mapumziko ya siku mbili kwa wachezaji ambao hawajaitwa timu ya Taifa, Taifa Stars, huku wale walioitwa walipumzika siku moja kwa maana ya Jumapili (juzi) na Jumatatu (jana) wanakwenda kuungana na wenzao.

“Tunatarajia Jumanne wachezaji wote watafika klabuni kwa wakati wakiwa na viongozi wa benchi la ufundi na kupelekwa kambini kujiandaa na mechi inayokuja dhidi ya Simba,” alisema Bumbuli.

Wakati huo huo, BINGWA limetonywa kuwa kabla ya pambano lao na Simba, Yanga itacheza mechi mbili za kirafiki ili kuwaweka fiti wachezaji wao.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *