Posted By Posted On

Chelsea waonyesha jeuri ya fedha

LONDON, England

TIMU za Ligi Kuu England zimetumia kitita cha pauni bilioni 1.24 kufanya usajili katikia dirisha lililofungwa hivi karibuni, huku ikidaiwa klabu nyingi ziliyumba kiuchumi kutokana na janga la virusi vya corona.

Hata hivyo, kiasi cha pauni milioni 160 kilikuwa pungufu ya pesa iliyotumika msimu uliopita, lakini ni zaidi ya pauni milioni 70 ambazo zilitumika katika dirisha la msimu wa 2016.

Chelsea wanakamata usukani kuwa timu iliyotumia pesa nyingi katika dirisha hili. Wakali hao wa Stamford Bridge wametumia paundi milioni 226.

Chelsea walifanikiwa kunasa saini za Timo Werner, Hakim Ziyech, Edouard Mendy na Ben Chilwell. Huku Kai Havertz akiwa mchezaji ghali zaidi katika dirisha hili la usajili baada ya kuwasili akitokea Bayer Leverkusen.

Manchester City wapo nafasi ya pili, wao wametumia pesa zao kwa kupata huduma za kina Nathan Ake na Ferran Torres, lakini baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 5-2 kutoka kwa Leicester City. Pep Guardiola aliingia sokoni na kumsajili beki Ruben Dias kutoka Benfica.

Aston Villa walijibu mapigo kwa kutumia zaidi ya pauni milioni 85 huku usajili wa straika Ollie Watkins ukioneka kuwa bora na mzuri kwao.

Leeds United inayofundishwa na Marcel Bielsa hawakupoteza muda, baada ya kureja Ligi Kuu England walitoa pesa na kusajili wachezaji kama Rodrigo, Robin Koch, Raphinha na Diego Llorente.

Wolves waliendelea kuongeza wachezaji raia wa Kireno kwenye kikosi chao kwa kuwashusha Fabio Silva na Nelson Semedo, huku wengine ni Marcal na Ki-Jana Hoever.

Wanaofuata ni Liverpool, ambao walitumia pauni milioni 45 kumsajili Diogo Jota, pauni milioni 27 kwa Thiago Alcantara na pia kumsajili Kostas Tsimikas.

Arsenal walimwaga pesa kwa Thomas Partey kutoka Atletico Madrid, Gabriel Magalhaes na Runar Alex Runarsson.

Everton walitumia pauni milioni 65 kunasa saini za wakali wapya  ambao wamerudisha makali ya timu hiyo wakiwamo Allan na Abdoulaye Doucoure huku Tottenham wakitumia pauni milioni 62 kupata huduma ya Pierre-Emile Hojbjerg na Sergio Reguilon.

Manchester United walitumia pauni milioni 54.4 kuwasajili Donny van de Beek na Alex Telles huku wengine ni Facundo Pellistri na Amad Diallo.

Leicester City, usajili wao mkubwa ulikuwa ni Timothy Castagne huku jumla wakitumia pauni milioni 51.5 nao Newcastle United walitoa pauni milioni 35 kupata saini za Callum Wilson na Jamal Lewis.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *