Posted By Posted On

CRDB yadhamini ligi ya taifa mpira wa kikapu

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya CRDB imetangaza udhamini wa Sh milioni 200 kwa ligi ya kikapu ya taifa  itakayofanyika Dodoma  kwenye viwanja vya Chinangali kuanzia Novemba 12- 21,  mwaka huu. 

Akizungumza jana Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully  Mwambapa, alisema benki hiyo imefikia makubaliano na Shirikisho la Taifa la Mpira wa Kikapu (TBF) kutoa udhamini wa ligi hiyo ambayo imepewa jina la ‘CRDB Bank Taifa Cup’.

Mwambapa alisema udhamini wa ligi hiyo ni mwendelezo wa jitihada za Benki ya CRDB katika kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupitia michezo. 

Alisema benki hiyo kupitia sera yake ya Uwezeshaji katika Jamii (CSI Policy) imekuwa ikiwekeza katika michezo ya vijana kwa kuamini kuwa inasaidia kuongeza ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii.

Akizungumzia kuhusu msukumo uliochangia benki hiyo kudhamini ligi hiyo yenye kaulimbiu ya ‘Ni Zaidi ya Game, Ni Maisha’, Mwambapa alisema mchezo wa mpira wa kikapu umekuwa haupewi kipaumbele kulinganisha na michezo mingine, hivyo kuwakatisha tamaa vijana wengi ambao wamekuwa wakionyesha vipaji katika mchezo huo.

“CRDB Bank Taifa Cup inakuja kuleta hamasa si tu kwa vijana na wapenzi wa mpira wa kikapu bali kwa Watanzania wote kwa kuwaonyesha umuhimu wa kuwekeza katika michezo ya vijana na fursa zilizopo ikiwamo ajira,” alisema Mwambapa.

Mwambapa alisema mbali na zawadi zitakazokuwa zikitolewa kwa timu zitakazofanya vizuri Benki ya CRDB, pia imetenga Sh milioni 50 kwa ajili ya ‘Scholarship’ kwa wachezaji watakaofanya vizuri. 

“Tutakuwa pia na zawadi kwa ajili ya wapenzi wa mpira wa kikapu katika kila hatua za mashindano. Niwaombe Watanzania waanze kutufuatilia kupitia Azam TV na mitandao yetu ya kijamii kujua namna ya kushiriki,” alisema.

Kwa upande wake,  Katibu Mkuu wa TBF, Mike Mwita, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kudhamini ligi hiyo na kusema udhamini huo utaongeza mapenzi ya mpira wa kikapu kwa vijana kama ilivyo kwa soka na michezo mingine. 

“Tunafurahi kwa udhamini na ushiriki thabiti wa Benki ya CRDB katika jitihada hizi zinazolenga kukuzwa kwa mpira wa kikapu nchini. Udhamini wa Benki ya CRDB utaboresha kiwango cha ligi pia utavutia Watanzania wengi kufuatilia mchezo huu na kuhamasisha vijana wengi kushiriki,” alisema Mwita.

Naye Msimamizi wa vipindi vya michezo Azam TV, Michael Maluwe, aliwataka Watanzania kuanza kufuatilia CRDB Bank Taifa Cup kupitia chaneli ya michezo ya Azam Sports 2, ambapo benki hiyo imeanzisha kipindi maalumu kuelekea mashindano hayo.

“Azam TV itaweka kambi Dodoma kuwaletea burudani Watanzania kuelekea mashindano haya, niwakaribishe Watanzania ili kuwashangilia vijana wetu,” alisema Maluwe.

CRDB Bank Taifa Cup inatarajia kushirikisha timu 36 kwa upande wa wanaume na wanawake.

Ligi hiyo itatanguliwa na michuano ya timu za veteran za Benki ya CRDB, Bunge, Pazi, Bahari na timu za walemevu. 

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *