Posted By Posted On

YANGA NI KICHEKO TU

NA ASHA KIGUNDULA

YANGA ni kicheko tu, ni baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba  uliopangwa kuchezwa Oktoba 18, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kupelekwa mbele.

Kwa sasa mchezo huo umepangwa kuchezwa Novemba 7, mwaka huu, huku Yanga wakifurahishwa na uamuzi wa Bodi ya Ligi Tanzania  wa kufanya hivyo, ambao utawapa muda wa kuandaa kikosi chao hasa baada ya kumtimua kocha wao, Mserbia Zlatko Krmpotic kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Zlatko aliyetua Yanga kuchukua nafasi ya Luc Eymael alikiongoza kikosi hicho  katika michezo mitano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akishinda minne na sare moja, lakini mapema wiki hii alikatishiwa mkataba wake na uongozi wa klabu hiyo

Kabla yake uongozi wa klabu hiyo, uliomtimua Eymael baada ya kumalizika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara,  akionekana ni mtovu wa nidhamu kwa kutoa Lugha ya kibaguzi.

Hata hivyo,  kitendo cha Bodi ya Ligi kupeleka mchezo huo mbele kutaiwezesha Yanga kujipanga vyema dhidi Simba ikiwa na kocha mpya anayetajwa kutua muda wowote katika klabu hiyo, raia wa Burundi Cedric Kaze.

Ikumbukwe kwamba mchezo mwisho wa nusu fainali wa michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, alisema wamefurahi mchezo huo kupigwa kalenda, kwani kocha wao mpya atapata nafasi ya kuandaa kikosi cha maangamizi.

Nugaz alisema anaamini wiki mbili zitamtosha kocha wao mpya anayetarajiwa kutangazwa kufanya maandalizi kwa kikosi kitakachovaana na Simba na baadaye kuibuka na ushindi.

Alisema wanachama na mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuwa watulivu na amani, kutokana na taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi, ambayo itasaidia timu yao kufanya maandalizi mazuri ya mchezo huo.

Alisema pamoja na mabadiliko ya mchezo huo, wachezaji wao  walikuwa wameanza kambi  kujiandaa na mtanange wao uliopangwa kuchezwa Oktoba 18, mwaka  huu.

 “Tumepokea taarifa ya Bodi ya Ligi kwa furaha na vyema kila timu ikawa na vikosi kamili, ni jambo jema kwa Bodi ya Ligi kuliona hilo, kwetu sisi tunapata maandalizi mazuri zaidi,  hata kocha wetu akija atakuwa na wiki mbili za kukinoa vizuri.

 Yanga tumepokea kwa mikono miwili mabadiliko hayo na watu wasilaumu, ratiba imebadilika twende mbele,” alisema Nugaz.

Kwa upande wa Simba, Meneja wa kikosi hicho, Patrick Rweyemamu, alisema hawezi kuzungumzia zaidi, lakini anashangazwa na uamuzi wa kusogeza mbele mchezo huo.

Rweyemamu alisema sababu iliyotolewa na Bodi ya Ligi kuwa baadhi ya wachezaji wa timu hizo ambao wameitwa kwenye vikosi vya taifa vya nchi zao haina mashiko.

Alisema  katika kikosi chao wachezaji wa kigeni waliondoka ni  beki Joash Onyango na kiungo Francis Kahata ambao wamekwenda kuitumikia timu yao ya taifa ya Kenya, Harambee Stars inayokabiliwa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa, hivyo haiwezi kuwa sababu ya kusogeza mbele mchezo huo.

“Mimi  nimeona mabadiliko hayo kupitia mtandao, lakini imeshangaza kidogo, maana Yanga haina mchezaji wa kigeni aliyeondoka nchini kwenda kwenye timu ya Taifa, Simba wameondoka wachezaji wawili, kusema ukweli sababu haina mashiko kabisa.” alisema Rweyemamu.

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Tanzania ya jana kwa kupitia Mtendaji Mkuu  wake, Almas Kasongo, mabadiliko ya ratiba ya mchezo huo, yanatokana na kikwazo cha usafiri kwa wachezaji wa kigeni waliokwenda kwenye timu zao za taifa,wakati watakaporejea nchini kutokana na hali ya ugonjwa wa Covid19.

Taarifa hiyo ilisema kutokana na kuwapo kwa janga la Covid19, baadhi ya nchi zenye wachezaji wa timu hizo, wanaweza kuathiri vikosi vyao vya Yanga na Simba kwa kukosa usafiri wa kurejea nchini.

Ilisema baadhi ya nchi zimeendelea kuweka masharti maalum ya utaratibu za usafiri kimataifa tangu kuzuka kwa janga la hili.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *