Posted By Posted On

Amri Said akalia kuti kavu Mbeya City

NA ZAINAB IDDY KOCHA wa timu ya Mbeya City, Amri Said, amekalia kuti kavu baada ya kikosi chake kushindwa kupata matokeo ya kurithisha tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Mbeya City ambayo imenusurika kushuka daraja msimu uliopita  wa ligi na kuponea hatua ya mechi za mtoano haijaonja ladha ya pointi tatu. Timu hiyo ilianza ligi kwa kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa  vijana wa Kinondoni (KMC), kisha kuchapwa 1-0 na Yanga,  kabla ya kunyukwa bao 1-0 na Azam na baadaye kupigwa bao 1-0 na Namungo  na kutoka suluhu na Tanzania Prisons. Matokeo hayo yameiweka Mbeya City katika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi tano. Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Mbeya City, zinasema kuwa licha ya kikosi chao kuwa kipya msimu huu, lakini bado matokeo wanayoyapata hayastahili. “Sidhani kama Amri amebakiza muda mrefu ndani ya Mbeya City na sababu kubwa ni matokeo tunayopata, uongozi wanapambana kuipa kila kinachostahili, lakini bado hatuoni kitu kinachofanyika uwanjani. “Uongozi ukihoji sababu kubwa ya matokeo hayo unaambiwa ugeni wa wachezaji wengi kwenye timu msimu huu, lakini mbona msimu wa 2013/14 hatukuwa na mchezaji yeyote aliyewahi kucheza ligi na bado tulipata matokeo mazuri, mechi tano pointi moja hii haipo sawa.” Mtoa habari huyo aliongeza hata kama uongozi wa Mbeya City hautoamua kuachana na kocha, lakini wanavyommjua Amri hatoweza kuendelea kuona timu inapata matokeo hayo ataomba kuondoka mwenyewe. BINGWA lilimtafuta Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe,  kujua mipango yao baada ya matokeo yanayopatikana,  alisema ni sehemu ya mchezo.  “Kufungwa, kushinda na kupoteza ni sehemu ya matokeo ya mchezo,mpango wa kumuondoa Amri sababu ya matokeo haupo labda kama ataamua kuondoka mwenyewe.” Kimbe.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *