Posted By Posted On

BARBRA STREISAND:Mkali wa nyimbo za ‘kumtoa nyoka pangoni’ aliyezoa tuzo kibao

MICHAEL MAURUS NA MITANDAO

NI mwigizaji, mwimbaji, mwongozaji, mtunzi wa mashairi, mtayarishaji, msanifu, mshiriki na kiongozi wa kazi zake za kimuziki.

Kutokana na umahiri wake katika muziki, ubunifu na sanaa nyingine, amefanikiwa kutwaa tuzo nyingi zaidi ya msanii yeyote duniani.

Huyo ni Barbra Streisand, ambaye kutokana na mafanikio yake aliyoyapata kupitia kazi za kimuziki na ubunifu, alifanikiwa kushinda tuzo kibao, zikiwamo za Oscar, Tony, Emmy, Grammy na Golden Globe.

Pia, alitwaa tuzo ya National Endowment for the Arts na ile ya Peabody, ikiwa ni pamoja na tuzo aliyopewa na Chuo cha Filamu ya Marekani ya American Film Institute’s Lifetime Achievement.

Barbra pia ni msanii pekee mwongozaji wa filamu aliyetwaa tuzo ya Kennedy Center Honors.

Alitwaa tuzo ya Oscars kama mwigizaji bora wa kike na mtunzi bora wa nyimbo, filamu tatu alizoziongoza, zilipigiwa kura ya tuzo za Oscar mara 14.

Alitengeneza albamu zilizoshika nafasi ya kwanza katika ubora kwa miongo minne mfululizo na kuwa mwanamke aliyeuza zaidi kazi zake kuliko wote.

Kutokana na mafanikio yake katika muziki, alianzisha mfuko wake wa Streisand Foundation ambao ulimwingizia Dola za Kimarekani Milioni 700.

Katika maisha yake ya muziki na sanaa, Barbra amekuwa akibebwa zaidi na ubunifu wake wa hali ya juu, ambao ndiyo uliomfanya afikie alipo sasa.

Filamu ya “The Prince of Tides” ndiyo ya kwanza kuongozwa na mwanamke, iliyomfanya atwae tuzo ya mwongozaji bora.

Tangu wakati huo, mwanamuziki huyo aliendelea kujipatia umaarufu katika kila pembe ya dunia, huku akitwaa tuzo kemkem.

Albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la “The Barbra Streisand”, ilimwezesha kutwaa tuzo mbili za Grammy mwaka 1963.

Moja ya albamu hizo, ilitwaa tuzo ya kuwa albamu ya mwaka huo; wakati huo akiwa ni msanii chipukizi kuliko wote kutwaa tuzo.

Katika upande wa sinema, alishinda tuzo ya Academy ya mwigizaji bora kupitia kazi yake ya “Funny Girl”, mwaka 1968.

Nayo kazi yake ya “Yentl” ya mwaka 1983, ilimfanya kuwa mwanamke wa kwanza kutayarisha, kuongoza, kuandika na kuwa nyota katika filamu.

Babra anashikilia rekodi ya kuwa mtayarishaji mwanamke kushinda tuzo ya Academy, hiyo ilikuwa ni kupitia wimbo wake wa “Evergreen,” ambao ulikuwa ni chombezo katika filamu yake ya mwaka 1976 iliyotikisa vilivyo katika anga la filamu ya “A Star Is Born.”

Mwaka 1997 alichaguliwa tena kuwa mtunzi bora kupitia wimbo wake wa “I Finally Found Someone”.

Kipindi chake cha kwanza cha televisheni cha “My Name Is Barbra” (1965), kilimfanya atwae tuzo ya Emmy na ile ya Peabody.

Mbali na tuzo kemkem alizotwaa mwanamama huyo, pia alipewa medali ya sanaa na Rais Bill Clinton wa Marekani, iliyopewa jina la Tuzo ya Ubinadamu, ikiwa ni katika kampeni za Haki za Binadamu.

Heshima hiyo ilifuatiwa na nyingine nyingi kutoka kwa viongozi kadhaa wa ngazi za juu serikalini, ikiwamo ya Rais wa Ufaransa mwaka huo.

Barbra, alizaliwa Aprili 24, 1942 mjini Brooklyn, Marekani, mama yake akiwa ni Diana na baba, Emanuel Streisand.

Baba yake ambaye alifariki dunia wakati Barbra akiwa na umri wa miezi 15, alikuwa ni mwalimu anayeheshimika mno.

Barbra alipata elimu yake katika shule ya Erasmus iliyopo Brooklyn, na katika maisha yake ya kimuziki, alifanikiwa kufanya shoo kadhaa katika klabu, ikiwamo ile ya Manhattan.

Kutokana na umahiri wake, aliweza kuzivutia kampuni za muziki za Bon Soir na Blue Angel, ambazo zilionyesha nia ya kuwa naye.

Alisaini mkataba wa kufanya kazi na Columbia Records mwaka 1962, na albamu yake ya kwanza iliweka rekodi ya mauzo makubwa zaidi yaliyofanywa na msanii wa kike.

Baadhi ya kazi zake alizoziandaa ni pamoja na A Piece Of Sky, Being Alive, I Believe – You’ll Never Walk Alone, I’ve Finally Found Someone, If I Could, Love Light, Memory, No Matter What Happens, No Wonder (part I), No Wonder (part II) ba No Wonder (part III).

Nyingine ni People, Places That Belong To You, More Barbra Streisand, Some Good Things, The Rose, The Way I Feel, The Way We Where, This Is One Of Those Moments, Tomorrow Night, What Kind Of Fool, What Were We Thinking Of, Where Is It Written, Will Someone Ever Look At Me That Way, Woman In Love, You And Me Always na nyingine nyingi.

Huyo ndiye Barbra Streisand, mwanamama mwenye vipaji lukuki vya sanaa aliyetwaa tuzo nyingi kuliko mwanamke yeyote.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *