Posted By Posted On

CHAGUENI WENYEWE :*Simba watamba kupata kile walichokuwa wakikiota kwa miaka saba

NA MICHAEL MAURUS

KLABU ya Simba imesema kuwa kwa sasa haina presha yoyote ile kwani wamekipata kile walichokuwa wakikisaka kwa takribani misimu saba.

Tangu Simba ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2011/12, ilikuwa ikiishia kula kwa macho, ikilikodolea kombe likitua mara nne Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam, yaliko maskani ya watani wao wa jadi, Yanga na kubebwa mara moja na Azam.

Wekundu wa Msimbazi hao walizinduka msimu wa 2017/2018 waliporejesha umwamba wao kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kabla ya kufanya hivyo misimu miwili zaidi, yaani 2018/19 na 2019/20.

Kwa sasa mashabiki na wanachama wa Simba wamekuwa wakitembea vifua mbele kutokana na mafanikio hayo ya kubeba kombe la Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo, lakini ikiwamo kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2019/2019.

Katika kuonyesha uongozi wa Simba usivyotaka masikhara, umetamba kuendelea kulibeba kombe hilo la Bara msimu huu, ikiwamo kufika nusu fainali au fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mohammed Dewji, unaamini hakuna la kuwazuia kufikia malengo yao hayo kwani walijipanga kwa muda mrefu.

Akizungumza na BINGWA jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salum Abdallah ‘Try Again’, alisema kuwa baada ya kunyanyasika kwa muda mrefu, walikaa na kujipanga kuona ni vipi wanarejesha ufalme wao katika soka la Tanzania.

Alisema kwa muda mrefu walikuwa wakifikiria ni vipi wanakuwa na kikosi cha wachezaji wa kiwango cha kimataifa ambao watawapa mataji na kucheza soka maridadi la asili ya klabu yao.

“Toka tulipopoteza ufalme wetu (2012/13-2016/17), tulikuwa na ndoto ya kuwa na kikosi cha wachezaji wa kiwango cha kimataifa ambao wangecheza soka la asili ya Simba, soka la pasi la kuwapa mashabiki burudani na ushindi.

“Hatimaye tumepata wachezaji wa aina hiyo, tulikuwa nao msimu wetu wa kwanza kutwaa ubingwa wa ligi (2017/18) na misimu iliyofuata. Ila kwa msimu huu, tumepata aina ya wachezaji wanaoendana na falsafa ya klabu ya Simba.

“Ni wachezaji wenye vipaji vya mpira wa kiwango cha kimataifa. Sote tunaona mpira unaochezwa na wachezaji kama Luis Miquissone, Chama (Clatous), Mkude (Jonas), Kahata (Francis), Dilunga (Hassan) na hata mabeki kama Kapombe (Shomari), Pascal Wawa na wenzao… hawa ndio wachezaji wanaolingana na falsafa ya uchezaji ya Simba.

“Msimu huu tumeongeza nguvu kwa kuwaleta Larry Bwalya, Chris Mugalu, Bernard Morrison Joash Onyango na wazawa, Ame (Ibrahim) na wenzake…hawa ndio wachezaji wa aina ya Simba. Kwa kuwa na wachezaji wa aina hii, usitarajie butua butua, ni pasi tu,” alisema.

Alisema kwa muda mrefu, waliwakosa wachezaji wa aina hiyo ambao mbali ya kuwahakikishia ushindi katika mechi zao, pia watawapa mashabiki na wanachama wa Simba burudani ndani ya dakika 90 za mchezo kama ilivyo jadi yao.

Alisema kuwa kwa kikosi chao cha sasa, hawaoni kama kuna timu inaweza kuwazuia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu ya hivi karibuni, lakini pia wakiwa na uhakika na burudani ya nguvu kila pale timu yao itakapokuwa ikishuka dimbani.

Toka ligi hiyo imeanza, pamoja na kupata ushindi, kikosi cha Simba kimekuwa kikionyesha kandanda murua na la hali ya juu kiasi cha kuwapa raha wapenzi wao.

Miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa kivutio kwa Wanasimba, wakitamani kuwaona wakicheza kila siku ni Luis, Bwalya, Morrison, Chama, Mkude, Wawa, Onyango, Mugalu, Meddie Kwgere, nahodha John Bocco, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na wengineo.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *