Posted By Posted On

MWAMBUSI AWEKA MIKAKATI MIZITO KUIFANYA YANGA IWE TISHIO

Msomaji wa Yanganews Blog:Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kupisha kalenda ya kimataifa ya FIFA, benchi la ufundi la Yanga limeamua kuongeza programu ya mazoezi kwa lengo la kuimarisha wachezaji wake.

Yanga itashuka tena dimbani Oktoba 22, mwaka huu kuwakaribisha ‘Maafande’ wa Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini, Dar es Salaam.

Akizungumza na chanzo chetu hapo jana, Kocha Msaaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema amelazimika kuongeza muda wa kufanya mazoezi kwa sababu anahitaji kuona wachezaji wote wanakuwa fiti na tayari kucheza kwa dakika 90.

Mwambusi alisema licha ya kutopoteza mechi yoyote ya ligi katika raundi tano walizocheza, bado nyota wao hakuwa imara kama inavyotakiwa wakati msimu mpya unaanza.

“Tulikuwa tunafanya mazoezi mara moja, lakini sasa tutafanya mara tatu kwa siku, hii ni kwa ajili ya kukijenga kikosi kuwa fiti zaidi ili kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zinazofuata, tunataka kuwa na kikosi kilichoimarika,” alisema Mwambusi.

Kocha huyo alisema msimu huu umekuwa na ushindani zaidi tofauti na hali aliyokutana nayo miaka ya nyuma alipokuwa na timu nyingine kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 18 kutoka mikoa mbalimbali.

“Msimu huu ni mgumu zaidi kuliko kipindi chote ambacho nimewahi kufundisha timu Ligi Kuu, ligi imekuwa na ushindani mkubwa hali iliyosababisha nibadilishe programu ya mazoezi, sasa hivi tutafanya mazoezi mara mbili hadi tatu kwa siku,” alisema kocha huyo.

Aliongeza mpira wa sasa ni sayansi na wanahitaji kujipanga vizuri kwa lengo la kuhakikisha wachezaji wanaimarika na kufikia kwenye kiwango anachokihitaji.

“Sio kila siku tutafanya mazoezi mara tatu, inategemea na siku kulingana na programu, sababu kubwa ni kutopata muda wa kutosha wa kufanya maandalizi ya msimu mpya, wachezaji wengi wao ni wapya, hivyo hawakupata muda wa kukaa pamoja na kuzoeana uwanjani, muda huu wa kalenda ya FIFA ndio muafaka wa kufanya mazoezi ya nguvu na kuendelea pale tulipoishia.

“Huu sio muda wa kupumzika au kulala, tunatakiwa kupiga kazi kuhakikisha wachezaji wote wanakuwa fiti na tayari kwa ajili ya michezo iliyopo mbele yetu bila kujali tunakutana na timu gani,” alisema Mwambusi.

Aliongeza mbali na mazoezi ya uwanjani, pia amekuwa na ratiba ya kuzungumza na wachezaji wao kwa kuwakumbusha mambo muhimu wanayotakiwa kuyazingatia ili kufikia malengo yanayotarajiwa na viongozi pamoja na wanachama wa klabu hiyo.

Alieleza katika kuendelea kujiimarisha, kikosi chake kitacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mwadui FC kutoka Shinyanga itakayochezwa leo usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini.

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *