Posted By Posted On

Yanga yaja na mikakati ya hatari

Imelenga mambo matatu bab kubwa, sasa nyie endeleeni na neno lenu ‘tunawakera’ muone

NA ZAINAB IDDY

KLABU ya Yanga imekuja na mikakati ya hatari inayolenga kuwapa raha mashabiki na wanachama wao, huku pia ikilenga kuwakata ngebe watani wao wa jadi, Simba.

Yanga imeshindwa kutamba Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita, wakiwakodelea macho Simba wakibeba ‘mwali’ mara zote hizo.

Kwa kufahamu kilio cha mashabiki na wanachama wao, uongozi wa Yanga umekuja na mikakati mipya  yenye lengo la kutwaa mataji ya mashindano yote watakayoshiriki msimu huu katika ardhi ya Tanzania.

Katika kuhakikisha mikakati na malengo yao yanatimia, uongozi wa Yanga umeibuka na msimamo mmoja madhubuti ambao ndio hasa silaha ya mafanikio ya mtu, kampuni au taasisi yoyote ile.

Msimamo huo si mwingine bali ni suala zima la nidhamu kuanzia kwa viongozi, mashabiki, wanachama na zaidi wakiwa ni wachezaji wao, iwe ni ndani au nje ya uwanja.

Mara ya mwisho Yanga kutwaa taji la Ligi Kuu Bara ilikuwa ni msimu wa 2016/17 pale walipoongoza ligi wakiwa na pointi 68 sawa na Simba, lakini Wanajangwani hao walibebwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.

Tangu hapo, Yanga haijawahi kunyanyua kombe la ligi hiyo wala lile la Kombe la Shirikisho, hivyo kujikuta wakiishia kula kwa macho.

Kutokana na kiu kubwa ya Wanayanga kutaka kurejesha furaha waliyoikosa kwa misimu mitatu mfululizo, Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Dk. Mshindo Msolla, imekuja na mikakati mipya ya kuhakikisha wanatimiza hilo.

Mbali ya kulipa mishahara kwa wakati wachezaji na benchi la ufundi, lakini pia kwa kushirikiana na wadhamini wanaosimamia suala la usajili, kampuni ya GSM, imeiweka timu hiyo kambi nzuri katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.

Kama hiyo haitoshi, Mwenyekiti wa Yanga, Msolla akiwa sambamba na Makamu wake, Fredrick Mwakalebela, juzi jioni walitinga katika kambi ya wachezaji na kukaa chini na benchi la ufundi, kisha wachezaji, hiyo yote ikilenga kuwasisitizia vitu ambavyo hawataki vitokee msimu huu ambavyo vinaweza kukwamisha malengo waliyoyaweka.

“Wote tumewasajili tukiamini mna nidhamu nzuri na ya mfano, hivyo hatutavumilia vitendo vya aina yoyote vya utovu wa kinidhamu kutoka kwa mchezaji, lazima kuheshimu kanuni na taratibu tulizoweka kama klabu.

“Pamoja na nidhamu, mnatakiwa kujituma na kucheza kwa bidii ili kuipa timu matokeo yenye tija, hii ni kwaajili ya Yanga na hata mchezaji binafsi anayeweza kuonekana na timu nyingine nje ya Tanzania, tutakuwa tayari kumruhusu kwenda kufanya kazi kama tutakuwa na mkataba naye tukiamini mafanikio ya mchezaji, yanaihusu na klabu pia,” alisema.

Halikadharika, Msolla aliwatoa hofu wachezaji wao kuhusiana na mabadiliko ya benchi la ufundi yaliyofanyika hivi karibuni.

Wanajangwanin hao, hivi karibuni walitamngaza kuvunja mkataba na kocha mkuu wao, Zlatko Krmpotic na majukumu yake kubaki kwa Juma Mwambusi pamoja na Said Maulid ‘SMG’.

Msolla alisema mabadiliko ya makocha ni jambo la kawaida kwa timu inayohitaji mafanikio, hivyo wachezaji pamoja na makocha waliosalia wasiwe na wasiwasi.

“Kuondoka kwa kocha Krmpotic isiwe sababu ya kuwatia unyonge mliobaki katika benchi la ufundi, jambo la kujua uongozi tunawaamini na kuwaomba muendelee kufanya kazi vizuri kipindi tunamtafuta kocha mkuu mwingine.

“Kwa wachezaji, suala hili lisiwatie wasiwasi, mnafahamu kuwa timu inayohitaji mafanikio na katika kipindi cha kuijenga, lazima kuwe na hatua ngumu za kupita kama hizi, kuna wakati inapitia katika hatua ngumu kama hizi, endeleeni na majukumu yenu kwa kufuata miiko ya klabu,” alisema Msolla.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *