Posted By Posted On

Kaze atumia dk 90 kumaliza kazi Yanga

NA WINFRIDA MTOI

WANACHOSUBIRI Wanayanga kwa sasa ni kutangazwa kocha mpya wa kukinoa kikosi hicho ambaye tayari ameshajulikana ni Cedric Kaze, raia wa Burundi na ameanza kuandaa nondo za kuisuka timu hiyo.

Kaze alianza kutakiwa na Yanga kabla ya Zlatko Krmpotic, aliyefungashiwa virago hivi karibuni kutokana mwenendo wake usioridhisha uongozi.

Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo nchini Canada, akitarajiwa kutua wiki ijayo, amekuwa akitumia vitu mbalimbali vinavyoendelea katika kikosi hicho.

Yanga kwa sasa ipo chini ya kocha msaidizi Juma Mwambusi, alisaidiwa na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Said Maulid ‘SMG’ katika maandalizi ya mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wanajangwani hao wapo kambini kwa sasa na jana ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mwadui FC ili kuwaweka fiti wachezaji wake.

Taarifa ambazo BINGWA imezipata kutoka ndani ya Yanga, tangu alipopitishwa na uongozi wa klabu hiyo kuja kukinoa kikosi hicho, amekuwa akitumiwa kila kinachoendelea mazoezini.

Hata mchezo wa kirafiki wa jana alitumiwa ‘link’ ya kufatilia mwanzo mwisho mchezo huo ili anapotua jijini Dar es Salaam, iwe rahisi kwake kujua anaanzia wapi.

Kingine kinachofanyika  ili kumuwezesha  kocha huyo kuwa karibu na timu  hiyo kabla hajawasili nchini, ni kuwasiliana na kocha  Mwambusi  kuhusu maendeleo ya timu.

Yanga imeanza mazoezi mapema kuliko watani zao Simba kwa kuweka kambi ya moja kwa moja ikiwa ni maandalizi ya pambano lao na mechi nyingine za Ligi Kuu.

Wanangwani hao wataanza kuikabili Polisi Tanzania Oktoba 22, kabla ya kuivaa Simba Uwanja wa Mkapa.

Kutokana na muda uliotajwa wa kuwasili kwa Kaze ni wazi anaweza kuiwahi michezo yote miwili kwa sababu timu zipo katika mapumziko ya kupisha ratiba ya michezo kirafiki ya Kimatiafa ya vikosi vya Taifa.

Ofisa Mhamasishaji wa timu ya Yanga, Anthonio Nugaz, aliwataka mashabiki wa  klabu hiyo, kukaa mkao wa kula  kwani mambo mazuri yanakuja.

Nugaz alisema, muda wowote kocha mpya atatua nchini na atatangazwa hadharani kila  Mwanayanga atamuona na kumfurahia.

“Wanayanga tusiwe na wasiwasi kocha anakuja mwenye viwango kila mtu atamuona, wadhamini wetu chapa GSM, Taifa Gesi, Sportspesa wanahakikisha Yanga inakuwa bora,”alisema Nugaz.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga ipo nafasi ya tatu na pointi 13, ikishuka dimbani mara tano, imeshinda mechi nne na sare moja.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *