Posted By Posted On

LEO PATACHIMBIKA DIMBA LA MKAPA

Msomaji wa Yanganews Blog:Leo jioni kuna shoo moja matata wakati timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakapoikaribisha Ntamba Murugamba ambayo ni timu ya taifa ya Burundi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam katika mechi ya kirafiki kimataifa.

Pambano hilo linalotambuliwa kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa), litapigwa saa 10 jioni likiwa la kwanza kwa timu hizo za taifa kuumana tangu kuibuka kwa corona, ambapo timu zote mbili zimewaita mastaa wa maana kwenye mchezo huo.

Maproo wote wa Stars wanaocheza nje ya nchi soka la kulipwa wametua nchini isipokuwa Himid Mao wakiungana na wachezaji wanaocheza ligi za ndani kwa ajili ya mchezo huo.

Hawa hapa maproo wa Tanzania ambao wanatarajiwa kuonyesha makali yao kwenye mchezo huo wa kirafiki.

MBWANA SAMATTA

Samatta anayecheza soka la kulipwa Uturuki kwenye klabu ya Fenerbahce, ndiye mshambuliaji hatari zaidi kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Anaweza kuwa mchezaji ambaye atakuwa akitazamwa zaidi na mabeki wa Burundi kutokana na mambo makubwa ambayo amekuwa akiyafanya barani Ulaya.

Licha ya kutofanya vizuri akiwa na Aston Villa ya Ligi Kuu England, Samatta anaonekana kurejea kwenye makali yake.

Mshambuliaji huyo alithibitisha hilo Oktoba 3, 2020 kwenye mchezo wake wa kwanza kuanza kwenye kikosi cha Fenerbahce dhidi ya Fatih Karagumruk ambapo alitupia mabao mawili yaliyoipa timu yake pointi tatu za mchezo huo.

SAIMON MSUVA

Ukimuondoa Samatta, Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa Morocco kwenye klabu ya Difaa El Jadida ni mchezaj mwingine wa Kitanzania ambaye amekuwa akiipeperusha vyema bendera ya nchi nje ya nchi. Huu ni msimu wake wa tatu anacheza soka la kulipwa nchini humo na amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa barani Ulaya, ikiwemo Le Havre ya Ligi Daraja la Kwanza nchini humo maarufu kama Ligue 2.

Msuva amefunga mabao matano msimu huu kwenye ligi ya Morocco na amekuwa akifanya vizuri akicheza kama mshambuliaji wa mwisho akicheza na Samatta au kutokea pembeni.

THOMAS ULIMWENGU

Unaweza kusema kuwa Ulimwengu ndiye mchezaji ambaye ameanza kuonja utamu wa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye kikosi cha sasa cha Taifa Stars.

Tofauti na Msuva pamoja na Samatta, Ulimwengu hakuwahi kucheza Ligi Kuu Bara, amekuwa mtu wa kupasua anga japo mambo yameonekana kutomnyookea kama ilivyo kwa wenzake. Kwa sasa yupo TP Mazembe na ameuanza msimu mpya wa Ligi Kuu nchini humo ambapo wamecheza mchezo mmoja ambao walitoka suluhu dhidi ya Blessing.

HIMID MAO

Panga pangua kwenye kikosi cha Enppi huko Misri lazima utamuona Himid Mao ‘Ninja’ akianza kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku akitumika kama kiungo mkabaji.

Kukosekana kwake kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kunaweza kusababishwa na mambo mawili ambayo ni majeraha au kocha aamue ampumzishe. Himid ambaye alianza kucheza soka la kulipwa nchini Misri akiwa na Petrojet kabla ya kushuka daraja, ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa wakitegemewa na Kocha Helmi Toulan kwenye kikosi chake.

TANZANIA

Metacha Mnata (Yanga), Aishi Manula (Simba), David Kissu (Azam), Shomary Kapombe (Simba), Bryson David (KMC), Bakari Mwamnyeto (Yanga),Abdallah Sebo (Azam) na Dickson Job (Mtibwa Sugar). Wengine ni Iddy Mobbi (Polisi Tanzania), Jonas Mkude (Simba), Himid Mao (ENPPI, Misri), Simon Msuva (Difaa El Jadida, Morocco), Ditram Nchimbi (Yanga), Feisal Salum (Yanga). Ally Msengi (Stellenbosch, Afrika Kusini), Mbwana Samatta (Fenerbahce, Uturuki), John Bocco (Simba), Mzamiru Yassin (Simba), Iddy Nado (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo). Nickson Kibabage (Difaa El Jadida, Morocco), Said Hamis (Simba) na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam).

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *