Posted By Posted On

Carlinhos akiona cha moto

NA ZAINAB IDDY

NYOTA wa Yanga, Carlos Carlinhos, anakiona cha moto kwa kupigishwa tizi bab kubwa kama sehemu ya kumjenga zaidi kama ilivyopendekezwa na kocha mtarajiwa wa timu hiyo, Cedric Kaze.

Akizungumza na BINGWA jana, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, alisema kuwa wameamua kumpa programu maalumu ya mazoezi Carlinhos ili aweze kuwa fiti kwa asilimia 100.

Carlinhos ambaye ameirejesha Yanga kipindi cha Andrey Coutinho na Ibrahim Ajib kutokana na kupiga mipira mirefu, kona na adhabu za hatari, amekuwa kipenzi cha Wanayanga kutokana na uwezo wake huo.

Mwambusi alisema mchezaji wao huyo licha ya kuifanyia kazi kubwa na nzuri Yanga, lakini bado hajawa fiti kimwili jambo linalomkwambisha kutoa vitu vingi alivyonavyo.

“Carlinhos ana vitu vingi vizuri, lakini bado hajawa katika kiwango bora kutokana na muda mrefu alikuwa nje ya uwanja. Baada ya kugundua hilo, tumeamua kumpa programu maalumu ya mazoezi itakayomjenga na kumweka mwili wake katika utimamu mzuri.

“Watu wengi wanadhani Carlinhos ni mzuri akicheza namba 10, lakini nimempa nafasi ya kucheza namba nane na sita zote ameweza kuzimudu vizuri.

“Tumegundua Carlinhos anatakiwa kuwa katika hali gani ili awe vizuri, programu ya mazoezi tuliyompa itamsaidia kumjenga na kumfikisha katika hatua ya kutoa alivyonavyo kwa asilimia 100,” alisema Mwambusi.

Imeelezwa kuwa Mwambusi pamoja na wachezaji wa Yanga, walifanya kikao kwa video na Kaze aliyewapa mwongoza wake pamoja na kutaka Carlinhos aongezewe dozi ya mazoezi.

Kwa mujib wa kutoka ndani ya Yanga, Kaze anatarajiwa kutua nchini Jumatano hii tayari kuanza kutoa nondo zae kwa kikosi cha Wanajangwani hao.

Akizungumzia kwa ujumla kikosi chake, Mwambusi alisema mpango uliopo kipindi hiki ambacho Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama ni kuwapa nafasi wachezajia mbao hawakuwa wakiipata kuonyesha kile walichonacho. “Katika mchezo wetu na Mwadui, wachezaji wengi ambao hawakuwa wakitumika katika ligi ndio ambao wametumika, tunawapa nafasi kuona wana kitu gani cha kukifanyia marekebisho ili wote wawe na kiwango kimoja cha ubora,” alisisitiza kocha huyo

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *