Posted By Posted On

PANGA HILOO YANGA

NA ZAINAB IDDY

WACHEZAJI watano katika kikosi cha Yanga, wametakiwa kujitathimini na kubadilika, kinyume na hapo, wataonyeshwa mlango wa kutokea ndani ya kikosi cha Wanajangwani hao kipindi cha usajili wa dirisha dogo.

Wachezaji hao ni Faridi Mussa na Wazir Junior waliosajiliwa msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja, huku wengine wakiwa ni Deus Kaseke, Abullaziz Makame na Juma Mahadhi ambao mikataba yao inakwenda ukingoni.

Wachezaji hao walipewa nafasi ya kucheza katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mwadui FC na kuonyesha kiwango kilichowakera mabosi wa Yanga waliolazimika kukaa kikao cha dharura kuwajadili.

Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga aliyekuwamo katika kiko hiko cha dharura (jina tunalo), alisema hawakuridhishwa na kiwango walichokionyesha wachezaji hao.

“Usajili tuliofanya Yanga umelenga kuwa na kikosi kipana ambacho kitatupa matokeo na kucheza mpira tunaohitaji, lakini imekuwa kinyume kwani wasipokuwepo wachezaji fulani tu, timu inapiga mpira butua butua.

“Mpira huu wa ovyo ndio uliosababisha tumuondoe kocha Zlatko Krmpotic, lakini pia hao hao wachezaji walidai hawapewi nafasi ya kucheza, Juma Mwambusi ameomba tumtafutie michezo ya kirafiki ili kuwapa nafasi, wanacheza mpira wa ovyo kabisa,” alisema.

Mtoa habari huyo aliongeza: “Kwa mpira uliochezwa na Mwadui, kuna maana gani ya kusema Yanga tuna kikosi kipana, kama sio kuwa na wachezaji wanaoongeza idadi ya watu katika timu?

“Tumekubaliana kuwapa michezo mitatu mingine na tutakwenda kambini kuzungumza nao kuwataka wajitathimini, kinyume na hapo, Desemba sio mbali tutawaondoa kipindi cha dirisha dogo iwe kwa mkopo au kuachana nao kabisa na kuangalia wengine walio bora zaidi.”

Kuhusiana na kiwango duni kilichoonyeshwa na wachezaji hao, Kocha Mwambusi, amesema bado anaamini wachezaji wake watabadilika kwa sababu wana vitu muhimu isipokuwa miili yao haijawa tayari. “Wapo ambao hawajacheza kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali, nayo inachangia kiwango kushuka, nina uhakika katika kipindi hiki kifupi, mazoezi tutakayokuwa tunayafanya, watakujwa kukaa sawa na wachezaji wote watakuwa kwenye ubora mzuri unaolingana,” alisema Mwambusi.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *