Posted By Posted On

Baraka The Prince humwambi kitu kwa Gwambina FC

‘SAWA’ ni wimbo mpya wa Baraka The Prince aka The Black African Prince ambaye jina lake kamili kwenye kitambulisho chake cha NIDA ni Baraka Andrew.

Ama kwa hakika Baraka The Prince ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa kukata kiu ya mashabiki wa Bongo Fleva.

Msanii huyo anayefanya vizuri kwasasa chini ya lebo yake ya Bana Music, anasema yeye si shabiki wa soka lakini anavutiwa zaidi na utani wa jadi wa timu kongwe za Simba na Yanga, na yeye ataishabikia timu inayoshinda.

“Nimekua kwenye mazingira za muziki zaidi na sio mpira ila napenda kufuatilia ule utani wa Simba na Yanga kwa hiyo kusema nashabikia timu fulani sitaweza ila kwasasa nitaipa sapoti timu yangu ya nyumbani Mwanza, Gwambina FC,” anasema Baraka.

Wiki iliyopita, Mbarouk Ogga maarufu Mubenga ambaye amejizolea umaarufu kutokana na kushiriki kuinua, kukuza na kusimamia vipaji vya wasanii kibao wa Bongo Fleva, alipatia mechi tatu kati ya tisa kwenye utabiri wake japo katika zile alizotabiri na kupatia matokeo yalikuwa tofauti.

                                                                        El Chapo         Baraka The Prince

JKT Tanzania v Ruvu Shooting                     1-1                   1-0

Biashara Utd v Ihefu                                      2-0                   1-2

KMC v Coastal Union                                    1-0                   1-1

Namungo v Kagera Sugar                               1-2                   0-2

Gwambina v Mtibwa Sugar                            1-1                   2-1

Azam FC v Mwadui                                       3-0                   1-0

Dodoma Jiji v Mbeya City                              1-0                   1-2

Prisons v Simba                                               0-3                   0-2

Yanga v Polisi Tanzania                                  3-1                   2-1

JUMATANO

JKT Tanzania v Ruvu Shooting

JKT Tanzania ilikuwa na siku mbaya ofisini katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba. Vijana wa Abdallah Mohammed ‘Baresi’ walizidiwa kila idara na kujikuta wakifungwa mabao 4-0. Kusimama kwa ligi kupisha kalenda ya FIFA inaweza ikawa habari njema kwa JKT Tanzania kujipanga upya. Mechi dhidi ya Ruvu Shooting inakuja wakati mzuri kwa JKT Tanzania kusaka ushindi. Ruvu Shooting wanarudi katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma walikopoteza kwa wenyeji Dodoma Jiji lakini safari hii kocha Charles Boniface Mkwasa anaimani matokeo yatakua mazuri licha ya kuonyesha kukerwa na timu yake kucheza mechi za saa nane mchana.    

Biashara Utd v Ihefu

Uwanja wa Karume uliopo Mara unaotumiwa na Biashara United bado unakarabatiwa lakini sifa moja wanaojivunia timu hii inayonolewa na Mkenya Francis Baraza ni kutopoteza mchezo wowote wanaocheza nyumbani msimu huu hata kama sasa wanatumia Uwanja wa Nyamagana uliopo Mwanza kwa muda. Wapinzani wao Ihefu FC bado wanasusua kwenye Ligi Kuu Bara tangu kupanda na uvumilivu uliwashinda hadi kuamua kuachana na kocha wao, Maka Malwisi, kufuatia kufungwa na Gwambina.  

KMC v Coastal Union

Walianza msimu vizuri lakini kasi ya KMC inaanza kupungua. KMC walidhani watapata pointi moja mchezo wao wa mwisho dhidi ya Polisi Tanzania lakini dakika za mwisho wakaruhusu bao tena wakicheza Uwanja wa Uhuru ambao ni uwanja wao wa nyumbani uliokuwa unawapa matokeo mazuri hususan mechi za awali. Vijana wa Habib Kondo watakua na shughuli pevu dhidi ya Coastal Union ambayo waliruhusu mabao matatu katika mechi yao dhidi ya Yanga. Kocha Juma Mgunda anakisuka polepole kikosi chake kilichoondokewa na baadhi ya wachezaji nyota na mapumziko ya wiki mbili yanaweza yakawa yamekuwa ya manufaa kwake.   

Namungo v Kagera Sugar

Wengi watakuwa wanajiuliza, nini mbaya na Namungo FC? Hii sio Namungo FC ya msimu uliopita ambayo haikupoteza mchezo hata moja nyumbani. Lakini msimu huu, tayari wameshacheza mechi tatu kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi na kupoteza mbili. Mashabiki wake watataka kuona Namungo inapata ushindi watakapowakaribisha Kagera Sugar. Ni dhahiri kwa Kagera Sugar, hii haitakua mechi rahisi ila kama vijana wa Mecky Mexime watacheza soka safi kama walilolionyesha dhidi ya Azam FC, watarudi Bukoba na pointi zote tatu. 

ALHAMISI

Gwambina v Mtibwa Sugar

Ushindi ambao Gwambina walipata dhidi ya Ihefu FC kabla ligi kusimama kupisha kalenda ya FIFA, ilichochea timu hiyo ya Mbarali kuachana na kocha wake Maka Malwisi. Je, Gwambina watamfukuzisha kazi kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila? Ni mapema mbo, hata hivyo kilicho muhimu kwa Gwambina ni kushinda na kujiongezea pointi tatu ili kupanda kwenye jedwali la msimamo wa timu za Ligi Kuu Bara. Gwambina ilitabiriwa kufanya vizuri msimu huu miongoni mwa timu zilizopanda, lakini hadi sasa wamefanikiwa kushinda mechi moja tu kati ya tano walizocheza. Mtibwa Sugar watakua wanasaka ushindi wa pili ugenini na benchi la ufundi itahitaji mbinu ya ziada kuondoka na pointi tatu Kanda ya Ziwa.

Azam FC v Mwadui

Mechi tano, pointi 15 ni ishara ambayo Azam FC wanatoa kwamba msimu huu wamedhamiria kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Bara. Azam FC ndiyo timu pekee ambayo imeshinda mechi zote hadi sasa na wako vizuri zaidi wanapocheza nyumbani huku tayari wakiwa wameshapachika mabao saba. Mwezi Septemba umekuwa mzuri kwa Aam FC ambapo straika wao mpya tegemeo, Prince Dube raia wa Zimbabwe, alitwaa tuzo ya mchezaji bora na tuzo ya kocha bora ikimwendea Aristica Cioaba wa Romanian. Je, Mwadui watahitimisha rekodi ya asilimia 100 ya Azam FC kutopoteza mechi msimu huu? Kocha Khalid Adam anayo shughuli pevu ya kuongoza timu yake kuondoka na pointi tatu au hata moja Azam Complex.     

IJUMAA

Dodoma Jiji v Mbeya City

Kocha Amri Said aliipatia Mbeya City pointi ya kwanza msimu huu baada ya kucheza michezo mitano akilazimisha sare ya kutofungana dhidi ya Tanzania Prisons. Ni matokeo ambayo anaamini yatafungua ukurasa mpya kwa Mbeya City katika kupambana kuondoka mkiani kwenye msimamo wa ligi. Mbeya City wapo ugenini kuwakabili Dodoma Jiji iliyopanda daraja na ambayo imeshinda michezo yote miwili kwenye uwanja wake wa nyumbani. Dodoma Jiji watataka kuendeleza pale walipoishia kabla ligi kusimama ambapo waliwafunga Ruvu Shooting mabao 2-0.

ALHAMISI OKTOBA 22

Prisons v Simba

Mara ya mwisho Simba kucheza mechi Nyanda za Juu Kaskazini ilikuwa dhidi ya Ifehu FC na waliondoka na pointi zote tatu. Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wanarudi tena huko lakini safari hii sio Mbeya ila mkoani Rukwa kucheza na wenyeji Tanzania Prisons. Awali mchezo huu ulikua uchezwe Oktoba 11 mwaka huu lakini ukahairishwa ili kupisha timu ya taifa kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki. Simba itakuwa inasaka pointi tatu ili kuendana na kasi ya vinara wa ligi Azam FC na watani zao Yanga ambao wamepania kuchukua ubingwa. Licha ya Prisons kuhamia Rukwa na kutumia Uwanja wa Mandela, bado hawajafanikiwa kupata ushindi. Katika mechi tatu za nyumbani, vijana wa Salum Mayanga wametoa sare mechi mbili na kupoteza moja.  

Yanga v Polisi Tanzania

Zlatko Krmpotic, raia wa Serbia, aliiongoza Yanga kushinda 3-0 dhidi ya Coastal Union lakini huo ndiyo ukawa mchezo wake wa mwisho kabla ya kufungashiwa virago. Kocha huyo alidumu takribani miezi miwili na uvumilivu uliwashinda mabosi wa Yanga kwani inadaiwa hawakufurahia namna timu ilivyokuwa inacheza. Cedric Kaze, raia wa Burundi, anatajwa kuja kuchukua mikoba Krmpotic lakini ni kocha msaidizi Juma Mwambusi ndiye anayetarajiwa kuongoza timu itakapocheza na Polisi Tanzania. Polisi Tanzania watawavaa Yanga wakiwa na kumbukumbu ya kuwalazimisha sare ya mabao 3-3 Uwanja wa Mkapa msimu uliopita.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *