Posted By Posted On

Hivi ndivyo Zidane alivyo Real Madrid

MADRID, Hispania

GARETH Bale alikuwa kituko ndani ya Real Madrid, lakini, kubwa zaidi hakuwa na mahusiano mazuri baina ya kocha wa timu hiyo Zinedine Zidane. Hata hivyo, si mchezaji wa kwanza kuingia matatani na kocha huyo raia wa Ufaransa.

Mchezaji huyo aliyerejea Tottenham kwa mkopo, anayelipwa mshahara wa paundi 600,000 kwa wiki, aligeukia kucheza mchezo wa gofu huku akiishia kukaa benchi ndani ya kikosi cha Real Madrid.

Uhusiano wake na Zidane ulivunjika, itakumbukwa kuwa Bale, alikataa kujiunga na kikosi cha Real Madrid kilichoenda kucheza mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City uliochezwa kwenye Uwanja wa Etihad.

Lakini, Bale si mchezaji wa kwanza wa Real Madrid kuzinguana na Zidane. Hawa hapa nyota saba kuanzia kwa James Rodriguez hadi Achraf Hakimi, waliowahi kupata joto ya jiwe la kocha huyo raia wa Ufaransa.

JAMES RODRIGUEZ

Msimu huu katolewa kwa mkopo kwenda Everton. Pia, Rodriguez alitolewa kwa mkopo wa miaka miwili katika kikosi cha Bayern Munich kabla ya kurejea Santiago Bernabeu msimu uliopita.

Lakini, tangu arejee Real Madrid msimu uliopita aliishia kucheza mechi 14 tu, pia, mchezo mmoja tu tangu ligi iliporejea baada ya janga la virusi vya corona.

Hata hivyo, haonekani kuhitajika ndani ya klabu hiyo Real Madrid wamemuweka sokoni, kama kuna timu inamuhitaji basi waende kumchukua.

Hivi karibuni, kiungo huyo raia wa Colombia alikaririwa akisema anacheza nafasi ambayo haimudu uwanjani, Zidane hampi nafasi ya kucheza namba 10 (nyuma ya mshambuliaji) huku akiwa huru uwanjani.

KEYLOR NAVAS

Kwa muda mrefu, Navas alikuwa mlinda mlango chaguo la kwanza katika kikosi cha Zidane.

Lakini, tangu Thibaut Courtois awasili kutoka Chelsea, kipa huyo raia wa Costa Rica alilazimishwa kuondoka Real Madrid na sasa yupo PSG.

Navas aliingia kwenye mzozo na Zidane baada ya kocha huyo kurejea ndani ya klabu hiyo Machi, 2019.

KOVACIC, CEBALLOS NA LLORENTE

Umoja wa viungo watatu ambao walioshindwa kutamba ndani ya kikosi cha Real Madrid. Mateo Kovacic, Dani Ceballos na Marcos Llorente hawana dalili za kurejea Santiago Bernabeu.

Watatu hao waliishi chini ya vivuli vya Toni Kroos, Luka Modric na Casemiro ambao wamekuwa mzizi wa mafanikio ya Real Madrid chini ya Zidane, bila kujali viwango vyao.

Kovacic alienda Chelsea, ambako anaonyesha kiwango bora na kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo katika eneo la kiungo ndani ya Stamford Bridge.

Ceballos yupo kwa mkopo katika kikosi cha Arsenal na ameimarika zaidi chini ya Mikel Arteta ambaye anashawishika kumsajili jumla kwenye timu hiyo yenye maskani kwenye Uwanja wa Emirates.

Na Llorente anaing’arisha safu ya kiungo ya wapinzani wao Atletico Madrid baada ya kulazimisha kuondoka ndani ya kikosi hicho cha mabingwa wa Hispania.

ALVARO MORATA

Morata alirejea Real Madrid baada ya kuwa na mafanikio mazuri wakati huo akiitumikia Juventus, lakini alitarajia kuwa straika tegemeo ndani ya Santiago Bernabeu.

Lakini, Zidane aliendelea kumtumia Karim Benzema kama straika tegemeo huku Morata akiishia kuwa mchezaji wa benchi.

Morata alijiunga na Chelsea, ambako hakufanya vizuri. Lakini, kwa sasa, anaongoza safu ya ushambuliaji ya Juventus, baada ya misimu miwili ya karibuni kuitumikia Atletico Madrid.

ACHRAF HAKIMI

Akiwa katika kiwango kizuri, beki huyo raia wa Morocco alipelekwa kwa mkopo wa miaka miwili katika kikosi cha Borussia Dortmund huku Dani Carvajal akiendelea kutamba upande wa kulia wa Real Madrid.

Baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Ujerumani, Zidane hakuonyesha nia ya kumuhitaji ndani ya Real Madrid baada ya msimu kumalizika.

Hakimi aliuzwa jumla kwenda Inter Milan baada ya msimu uliopita kumalizika.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *